August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Morocco isiyumbishe msimamo wetu’

Spread the love

DIPLOMASIA ya Uchumi kati ya Tanzania na Morocco isitumike kuyumbisha msimamo wa Tanzania katika harakati za kupigania uhuru wa Taifa la Sahara Magharibi, anaandika Pendo Omary.

Tangu wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi utawala wa Rais wa Jakaya Kikwete, Tanzania ilikuwa na msimamo wa kuunga mkono wa kuendelea kuitambua Sahara Magharibi kwenye  vyombo vya kimataifa vikiwemo; Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU).

Msimamo huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi (TASSG) wakati hapo kesho Mfame wa Morocco Mohamed VI anatarajiwa kuja Tanzania na ujumbe wa wafanyabiashara takribani 1000 huku pia akitarajiwa kuingia mikataba 16 na Tanzania.

Alphonce Lusako, Mratibu wa Haki za Binadamu TASSC amesema “tunaitaka serikali ya Tanzania isiyumbe katika msimamo wake kuhusu suala la Sahara Magharibi.

“Ikumbukwe kuwa, kwa miongo minne, Moroco imekuwa ikiikalia kimabavu Nchi ya Sahara Magharibi kinyume na sheria na taratibu za kimataifa.

“Sisi kama vijana wa Afrika ambao tunajali misingi ya utu, umoja na mshikamamo wa Afrika kamwe hatuwezi kulinyamazia suala hili na kuisalti ndoto ya wasisi wa Umoja wa Afrika waliosisitiza kuwa Afrika haiwezi kuwa huru hadi pale nchi zote za kiafrika zitakapokuwa huru,” amesema Lusako.

Hata hivyo, mwaka 1975 Mahakama ya Kimataifa ya Haki (International Court of Justice- ICJ) kwenye hukumu yake ilitambua kwamba, kinyume na madai ya Morocco, hakuna mahusiano yoyote yale ya kihistoria au ya kisheria baina ya Sahara Magharibi na Morocco yanayoweza kuinyima Sahara Magharibi haki ya kujitawala.

Hata hivyo, Morocco inatajwa kuendelea kuwashikilia wafugwa wa kisaiasa na wanaharakati katika magereza yaliyopo katika maeneo ya Sahara Magharibi yanayokaliwa na Moroco.

“Tumesikitishwa sana na kitendo cha Moroco kuendelea kupuuzia wito wa Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla wake wa kuipatia Sahara Magharibi haki yake ya kujitawala.

“Tunapinga vikali mbinu za Morocco kuendelea na hila mbalimbali ili kuzuia Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kura ya Maoni nchini Sahara Magharibi tangu ulipoudwa mwaka 1991,” anaeeleza Lusako.

Aidha, Noel Shao, Mratibu wa Mawasiliano kwa Umma, TASSC ameutaka Umoja wa Mataifa kutanua mamalaka ya MINURSO ili iweze kutazama masuala ya haki za binadamu kwenye maeneo ya Sahara Magharibi yanayokaliwa na Morocco.

“Tunautaka Umoja wa Mataifa kuharakisha mchakato wa kura ya maoni ya kuipatia Sahara Magharibi uhuru wake. Mika 40 ya ukoloni wa Morocco nchini Sahara Magharibi inatosha,” amesisitiza Shao.

error: Content is protected !!