May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mfahamu Luteni Kanali Damiba aliyemgeuka Rais Kabore, alipewa cheo mwezi uliopita, Aweka historia kuwa Rais wa 10 kumpindua mtangulizi wake

Spread the love

 

WAKATI Timu ya Taifa ya Burkina faso ikitinga hatua ya nane bora katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) huko nchini Cameroon, nyumbani kwao katika jiji la Ouagadougou Jeshi limemtimua madarakani Rais Roch Marc Christian Kaboré.

Ilianza kama fununu Jumapili tarehe 23 Januari mwaka huu, lakini ilipofika tarehe 24, wababe wa Rais huyo wakajitokeza mbele ya runinga ya umma na kutangaza kushika madaraka

Aliyekuwa nyuma ya usukani huo, sio mwingine ni msomi na mtaalaam wa mapambano ya ugaidi – Paul-Henri Sandaogo Damiba.

Damiba ametambulishwa katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana Runinga ya Taifa ya Burkina faso (RTB) kama Rais wa vuguvugu Patriotic Movement for Safeguarding and Restoration (MPSR), ambalo sasa linashikilia madaraka nchini humo.

LAKINI DAMIBA NI NANI?

Damiba ni luteni kanali mchanga kabisa katika Jeshi la wana – Burkinabè.

Tarehe 3 Disemba mwaka jana, Damiba aliteuliwa kuwa Kamanda wa mikoa mitatu ya kijeshi nchini humo.

Mikoa hiyo ambayo ilighubikwa na vihatarishi vya ugaidi, jukumu lake kubwa ilikuwa ni kusuka mfumo wa kupambana na ugaidi katika ukanda huo wa mashariki wa Burkina faso hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usalama katika mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou.

Aliteuliwa kushika wadhifa huo kwa amri iliyotiwa saini na Rais Roch Marc Christian Kaboré, ambaye alikuwa amepangua safu za uongozi wa kijeshi nchini humo.

Rais huyo alipanga upya uongozi huo ikiwa ni siku moja baada ya shambulio la kigaidi lililotokea katika mji wa Inata na kusababisha vifo vya watu 57.

Wakati shambulio hilo linatokea, tayari maandamano makubwa yalikuwa yameandaliwa kudai rasilimali zaidi kwa jeshi huku uongozi wa Rais Kaboŕe ukipingwa vikali.

Luteni Kanali Damiba, kama mmoja wa viongozi wengi wa kijeshi walioteuliwa mapema Desemba, ni mmoja wa wale ambao Rais wa zamani wa mpito Michel Kafando aliwaita ‘the Boys’ baada ya kusimama kidete kupinga mapinduzi ya serikali mwaka 2015 yaliyoongozwa na viongozi wa zamani.

Kikosi maalum cha ulinzi wa rais (RSP) kilivunjwa baadaye.

Luteni Kanali Damiba pia alikuwa ametoa ushahidi mwaka wa 2019 wakati wa kesi ya aliyekuwa kiongozi wa mapinduzi hayo, Jenerali Gilbert Diendéré.

Kwa mujibu wa mtandao wa lefaso.net, Burkina24), Paul-Henri Damiba alikuwa kamanda wa kitengo cha kupambana na ugaidi, kilichowekwa katika mji wa Dori.

Yeye mwenyewe ni mwanachama wa zamani kikosi cha RSP, akitoa ushahidi aliieleza mahakama kuwa mwaka wa 2015 alipokea simu kutoka kwa Jenerali Djibril Bassolé, ambaye alimuuliza kama anakuja kuongeza nguvu kwenye mapinduzi hayo jijini Ouagadougou.

SHULE YA VITA YA PARIS

Luteni Kanali Damiba pia ni mwandishi wa kitabu. Kitabu hicho kinachohusu ugaidi, kilichapishwa Juni mwaka jana kikiwa na jina la

‘West African Armies and Terrorism: Uncertain Answers?’

Luteni Kanali Damiba amechambua mikakati ya kukabiliana na ugaidi katika eneo la Sahel na mipaka ya nchi hiyo.

Katika machapisho yake kwenye safu za magazeti mbalimbali nchini humo na Ufaransa, yanaonesha kwamba Paul-Henri Sandaogo Damiba ni mhitimu wa shule ya kijeshi huko jijini Paris nchini Ufaransa.

Jina lake linaonekana kwenye baadhi ya magazeti hayo kuwa ni kati ya maofisa wa kigeni 24 waliohitimu kutoka Shule ya Vita, mnamo 2017.

Damiba ana shahada ya uzamili katika sayansi ya uhalifu kutoka katika Hifadhi ya Kitaifa ya Sanaa na Ufundi (CNAM) mjini Paris pia ana cheti cha utaalamu wa ulinzi katika masuala ya usimamizi, ukamanda na mikakati.

Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, Luteni-Kanali Damiba alikuwa akijishughulisha na operesheni kadhaa za kupambana na ugaidi kati ya 2015 na 2019 katika mikoa ya Sahel na Kaskazini mwa nchi hiyo.

NINI HATIMA YA BURKINA FASO?

Nchi hiyo iliyopata uhuru wake mwaka 1960, imekumbwa na zimwi la mapinduzi jambo linalodhihirisha kuwa kuna ombwe la uongozi makini.

Kwa sababu rais wa kwanza wa taifa hilo ambalo hapo awali lilikuwa linafahamika kama Upper Volta, baada ya uhuru mwaka 1960 Maurice Yameogo alichukua madaraka kwa katiba iliyokuwa inampa muongozo wa kutawala miaka mitano pekee.

Lakini apoingia madaraka alipiga marufuku vyama vya siasa nchini na muhula wake ulipoisha mwaka 1965 aliendelea kutawala taifa hilo, vyama vya wafanyakazi vilianzisha maandamano yasiyo na ukomo kwa kusaidiwa na Ufaransa kisha Jeshi likamtoa madarakani mwaka 1966.

Jeshi lilimteua Luteni Kanali Sangoule Lamizana aliyebaki madarakani kwa miaka minne hadi mwaka 1970 na kubadili katiba ambayo ilitoa muongoz wa kutawala miaka minne – minne.

Lamizana alichaguliwa tena mwaka 1978 lakini alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa vyama vya wafanyakazi ambapo mwaka 1980 aliondolewa madarakani kwa umwagaji wa damu na Kanali Saye Zerbo.

Kanali Zerbo naye alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa vyama hivyohivyo vya wafanyakazi kiasi cha kufurumushwa madarakani mwaka 1982 na Meja Dr. Jean Baptiste Ouedraogo.

Ouedraogo naye alikuja na mbinu za kupiga marufuku vyama vya siasa na vya wafanyakazi na kuondoa utawala wa kikatiba lakini naye akatimuliwa madarakani na Jeshi lililokuwa linamtii aliyekuwa waziri mkuu wake, Thomas Sankara.

Sankara alirejeshwa madarakani safari hiyo akiwa kama Rais, huku akiwa na rafiki yake wa karibu Kapteni Blaise Compaore ambaye aliongoza jeshi hilo kumrejesha madarakani Sankara mwaka 1983.

Sankara ambaye ni sawa na baba wa taifa hilo, alibadili jina la Upper Volta na kuwa Burkina faso, aliimarisha uhusiano wa kimataifa, kujenga shule, hospitali na huduma nyingine muhimu.

Alifungua uhuru wa kila mtu, kila chama cha siasa nchi hiyo ikawa moja ya nchi ya kuigwa Barani Afrika kwa maendeleo, lakini ghafla, rafiki yake wa karibu Sankara yaani Compaore alimng’oa madarakani na kusababisha kifo chake mwaka 1987

Compaore alitawala kwa mkono wa chuma kwa miaka 25 hadi mwaka 2014 alipong’olewa madarakani na maandamano makubwa yaliyokuwa yakipinga kiongozi huyo kubadilisha katiba na kujiongezea muda.

Tarehe 31 Oktoba, 2014 – Compaore alijuzulu na kuitisha uchaguzi ndani ya siku 90 huku akimuachia madaraka Yacouba Isaac Ziada ambaye alikuwa kama kiongozi wa mpito.

Tarehe 17 Novemba, 2014 Michel Kafando alichaguliwa kama Rais wa mpito na kuchukua madaraka ya Ziada.

Septemba mwaka 2015 kikosi cha usalama cha Rais, kilifeli kumpindua Rais Kafando ambaye aliwekwa kizuizini kwa siku saba kabla ya vyombo ulinzi vya kimataifa havijamrejesha madarakani kwa nguvu.

Ilipofika Oktoba mwaka 2015, kulifanyika uchaguzi na Roch Marc Christian Kabore akashinda kupitia chama chake cha Peoples Movement for Progres (MPP).

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 Kabore alishinda licha ya madai ya wizi wa kura.

Na sasa Kabore ameshikiliwa na Jeshi la nchi hiyo kutokana na madai mbalimbali ikiwamo kushindwa kudhibiti ugaidi nchini.

Luteni Kanali Damiba ndiye amechukua madaraka licha ya kwamba hatambuliwi na vyombo vyovyote vya kimataifa.

Makala haya yameandaliwa na GABRIEL MUSHI.

error: Content is protected !!