Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mfahamu Dk. Philip Mpango
Habari za Siasa

Mfahamu Dk. Philip Mpango

Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango
Spread the love

 

DAKTARI Phillip Isdor Mpango, mtaalamu wa masuala ya uchumi aliyependekezwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania na Rais Samia Suluhu Hassan, alizaliwa Jumapili ya tarehe 14 Julai 1957 wilayani Buhigwe mkoani Kigoma. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wasifu huo umetolewa leo tarehe 30 Machi 2021 bungeni jijini Dodoma, na Dk. Mpango, wakati anaeleze akijielezea mbele ya Bunge kabla ya kuthibitishwa na mhimili huo kuwa Makamu wa Rais.

Rais Samia amemteua Dk. Mpango kuirithi nafasi yake ya Makamu wa Rais, baada ya yeye kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, kufuatia kifo cha Hayati Dk. John Magufuli, aliyefariki dunia akiwa madarakani, tarehe 17 Machi 2021.

Dk. Magufuli alifariki dunia kwa ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam na mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi 2021.

Akielezea wasifu wake huo, Dk. Mpango amesema, safari yake ya elimu aliianza mwaka 1964 katika Shule ya Msingi Kipalapala mkoani Tabora.

Kisha 1965 alihamishiwa Shule ya Msingi Kasumo baadae alihitimishia elimu yake ya msingi katika Shule ya Muyama mkoani Kigoma 1970.

Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, mwaka 1971, Dk. Mpango alijiunga na masomo ya sekondari Shule ya Ujiji Seminary mkoani Kigoma ambako alisoma hadi 1975, akahamishiwa Shule ya Seminari ya Itaga mkoani Tabora alikomalizia masomo yake hayo mwaka 1977.

Kidato cha tano na sita alisoma katika Shule ya Ihungo mkoani Kagera kati ya mwaka 1976 hadi 1977.

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete

Baada ya kuhitimu masomo hayo, Dk. Mpango alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mkoani Kigoma na kambi ya JKT Mlale mkoani Songea.

Kati kati ya mwaka 1977 hadi 1981, Dk. Mpango alifanya kazi kwa muda mfupi katika Shirika la Taifa la Akiba ya Wafanyakazi (NPF), kisha akahamishiwa katika Shirika la Umma la Elimu Suppliers.

Mwaka 1981, alijiunga na masomo ya Shahada ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuhitimu 1984.

Baada ya kuhitimu UDSM, alifanya kazi katika Wizara ya Kazi, kwenye Idara ya ya Nguvu Kazi kuanzia 1985 hadi 1986, aliporudi tena chuoni hapo kuendelea na shahada yake ya pili ya uchumi.

Alipohitimu Shahada yake ya pili ya uchumi mwaka 1988 aliajiriwa chuoni hapo kufundisha akiwa Mhadhiri Msaidizi.

Mwaka 1990 hadi 1992, Dk. Mpango alijiunga na Chuo Kikuu cha Lund kilichopo nchini Sweden, na kufanikiwa kuhitimu Shahada ya Uzamivu (PhD)

Dk. Mpango alirejea nchini Tanzania 1992 kufanya utafiti hadi 1996 alipohitimu PhD ya Uchumi.

Baada ya kuhitimu PhD hiyo, Mpango aliendelea kufundisha UDSM katika Idara ya Uchumi hadi mwaka 2002, alipochukua likizo isiyokuwa na malipo.

Mwaka huo huo, Dk. Mpango aliajiriwa na Benki ya Dunia (WB) kama Mchumi Mwandamizi, nafasi aliyoitumikia kwa miaka mitano hadi 2007.

Dk. Philip Mpango, aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango akionesha begi lenye Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2019/20

“Nilienda sabbatical leave, nikaenda kufanya kazi Benki ya Dunia kama mchumi mwandamizi, haikuwa uamuzi mwepesi sana labda niwaambie kwamba niliamua kwenda kule ili nijifunze mataasisi haya makubwa ambayo yanasukuma sera na kwa nchi zetu yanafanyaje. Kuna nini kule ndani,” amesema Dk. Mpango.

Dk. Mpango mwenye miaka 63 amesema, alikuwa Katibu wa Kamati ya Mapitio ya Matumizi ya Umma ya Benki ya Dunia (WB).

“Nilifanya kazi pale na niliaminiwa kusimamia baadhi ya miradi hasa upande wa matumizi ya serikali, public expenditure review na mimi nilikuwa katibu wa ile timu ya benki ya dunia na serikali ambayo ilikuwa inaratibu zoezi hilo,” amesema Dk. Mpango.

Mwaka 2007 hadi 2010, Dk. Mpango aliteuliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete kuwa mshauri wake katika masuala ya uchumi.

Mwaka 2009 hadi 2010, Kikwete alimteua kuwa naibu katibu mkuu wizara ya fedha na mipango na mwaka 2010 hadi 2015, akamteua tena kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Tanzania.

Mara baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, kuingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015, alimteua kuwa Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Matapo Tanzania.

Nafasi hiyo, hakuhudumu kwa kipindi kirefu kwani mwaka huo huo, Novemba 2015, Dk. Mpango aliteuliwa Hayati Magufuli kuwa mbunge kisha Waziri wa Fedha na Mipango.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana 2020, Dk. Mpango aligombea Ubunge Buhigwe mkoani Kigoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kufanikiwa kushinda.

Baada ya kushinda uchaguzi huo, Dk. Magufuli alimetua tena kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, nafasi aliyohudumu hadi alipoteuliwa na Rais Samia kuwa Makamu wa Rais.

Dk. Mpango, anakuwa makamu wa Rais wa tano wa Tanzania, tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1995.

Waliomtanguliwa ni; Omar Ali Juma kuanzia mwaka 1995 hadi 2001 , alipofariki dunia na Dk. Ali Mohamed Shein, akashika kijiti kuanzia mwaka 2001 hadi 2010.

Mwaka 2010 hadi 2015, alikuwa Dk. Mohamed Gharib Bilal na mwaka 2015 hadi Machi 2019, alikuwa Samia Suluhu Hassan ambaye 19 Machi 2021, aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania, baada ya kifo cha Rais John Magufuli.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

error: Content is protected !!