August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Meya wa kihistoria aapishwa Dar

Spread the love

ISAYA Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, ameapishwa leo, akiwa meya wa 17 tangu mwaka 1949, anaandika Happyness Lidwino.

Mwita, Diwani wa Kata ya Vijibweni (Chadema), Kigamboni, ni meya wa kwanza wa jiji la Dar es Salaam asiyetokana na chama kinachotawala.

Kumbukumbu za Jiji zinaonesha orodha ya mameya waliomtangulia Mwita, huku baadhi yao wakiwa wameandikwa kwa jina moja tu au kwa vifupi vya majina yao ya kwanza.

Wengine wanaonekana walishika ofisi kwa muda mfupi; na wakati mwingine kulikuwa na mameya zaidi ya mmoja ndani ya mwaka mmoja.

Watangulizi 16 wa Mwita ni Pevirett Obi (1949-1952), Aya Kareemjee (1953-1955), T.W. Tyrrell (1955-1956), S.D Owarth (1957-1958), na. S.M.M. Devani (1959).

Wengine ni Ramadhan Nyamka (1978-1982), Kitwana Kondo (1983, 1995), A.A Abed (1991), M. Mfaume (1992-1993), R.O Kirundu (1994-1996), O.O Nondo (1997), A. Sambuso (1997), na Abuu Juma (1996-2000), Kleist A. Sykes (2000-2005), Adam O. Kimbisa (2005-2010), na Didas Massaburi (2010-2015).

Aziza Kalli, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Sokoine Drive, Dar es Salaam ndiye aliyemwapisha Mwita ili aanze majukumu yake rasmi.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwa meya ni Wilson Kabwe, Mkurugenzi Mkuu wa Jiji; Sarah Yohana, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji; Charles Kuyeko, Meya wa Manispaa ya Ilala, na Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo.

Baada ya kuapishwa Mwita amezungumza na vyombo vya habari akasema anadhamiria kuwa kiongozi muunganishi bila kujali tofauti za kiitikadi.

Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam akiapishwa
Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam akiapishwa

Amesema hatarajii kipindi chake cha uongozi kiwe na vurugu au machafuko katika Jiji la Dar es Salaam.

‘’Viongozi wangu wa chini wajisikie amani, kwani mimi nitakuwa kiongozi bora kwa watu wote. Wala sikuja kwa ajili ya kuleta machafuko na ugomvi, bali nahitaji amani ili tutafute maendeleo,’’ amesema.

Mwita amesisitiza ushirikiano kwa viongozi wote ili washughulikie changamoto za muda mrefu katika jiji hilo – usafiri, miundombinu, afya, elimu, na huduma nyingine za jamii.

Naye Kubenea amesema wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wamefurahishwa na kukamilika mchakato wa umeya ambao ulicheleweshwa na mizengwe ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kwa miezi minne mfululizo kilikwamisha uchaguzi wa meya, kikitafuta fursa ya kung’ang’ania madaraka ya uongozi wa jiji.

“Sasa ni wakati wetu wa kutumikia wananchi, na kusahihisha makosa na maovu yote yaliyofanywa na watangulizi wetu huko nyuma.

“Ni muda sasa wa kuanika mali za umma hadharani ili kila mwananchi azijue, kwani kuna mambo yalikuwa yakifanyika, ikiwemo kusaini mikataba feki gizani. Sasa yatawekwa hadharani. Wakwapuaji wa mali za umma wajiandae,’’ amesema Kubenea

Meya wa Manispaa ya Ilala ameahidi kushirikiana na Mwita katika kuleta maendeleo, hasa katika kusimamia ukusanyaji kodi. Amesema, “tumeahidi mengi kwa wananchi ambayo yote yanahitaji pesa, ambazo zipo kwa wananchi. Hivyo, ni ombi langu kwa wananchi wajitume kulipa kodi.”

Tukio hilo limehitimisha sekeseke la umeya lililodumu kwa miezi mitano mfululizo.

Uchaguzi wa Meya wa Jiji ulifanyika tarehe 22 Machi 2016,Mwita aliibuka mshindi kwa kura 84 dhidi ya Yusuph Omar wa CCM aliyepata kura 67.

error: Content is protected !!