July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Meya Silaa afungua soko linaloelea

Soko la Mtaa wa Kigogo Fresh 'B' kata ya Pugu likiwa limezingirwa na maji

Soko la Mtaa wa Kigogo Fresh 'B' kata ya Pugu likiwa limezingirwa na maji

Spread the love

MEYA wa Manispaa ya Ilaa, Jerry Silaa amefungua soko linaloelea kwenye maji, huku eneo lake lote likiwa limezungukwa na vichaka. Anaandika Pendo Omary …. (endelea).

Soko hilo ni la Kigogo Fesh ‘B’ lililopo kata ya Pugu, limefunguliwa jana huku ujenzi wake uliosimamiwa na halmashauri hiyo ukichukua takribani miaka tisa lakini haujakamilika kwa asilimia 100.

Maji hayo yanatokana na mvua zilizonyesha Mei mwaka huu. Hakuna miundombinu ya kupitisha maji taka. Pia soko halina umeme na maji safi. Hali inayohatarisha afya ya watumiaji wa soko hilo ambalo litabeba wafanyabiashara zaidi ya 200.

Akizungumza na wafanyabiashara waliopewa vibanda kwenye soko hilo katika mkutano maalum uliokuwa na lengo la kujua hatma ya soko hilo, Silaa amesema “nasema kuanzia leo soko hili limefunguliwa.”

“Tumieni mwezi mmoja wa mpito kupata orodha ya wafanyabiashara. Nitashirikiana nanyi kuchimba mtaro kupitisha haya maji. Leo nitawasiliana na wataalam, huku tukiendelea kuangalia ni hatua gani zifanyike kudhibiti mafuriko ndani ya soko,” amesema Silaa.

Silaa amechukua hatua hiyo baada ya ucheleweshaji wa ufunguzi wa soko hilo kuathiri wafanyabiashara ndogondogo hasa ambao waliondolewa pembeni mwa barabara ya kata hiyo, baada ya vibanda vyao kuvunjwa kwa ahadi ya kupewa vizimba katika soko hilo jipya.

“Aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa huo kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014, Ally Maguno, alitangaza kukamilika ujenzi wa vizimba vya soko hilo na kuruhusu biashara kuanza ndani ya siku 17. Hii ilikuwa Oktoba mwaka 2013.

Lakini wafanyabiashara hao walizuiwa wa manispaa hiyo, kwa kuwa ujenzi haujakamilika na lisingefaa kwa matumizi ya kibiashara.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Mwanaisha Abdu, mkazi wa mtaa huo anasema “Kwa muda mrefu tunanunua mahitaji Gongo la Mboto. Tunatumia muda mwingi na gharama kubwa kufika huko kununua mahitaji.”

Aidha, uchunguzi wa MwanaHALISI Online umebaini, kuchelewa kufunguliwa kwa mradi wa soko hilo kunatokana na umeme na maji kutounganishwa na soko hilo na mkandarasi bado anadai fedha zake.

error: Content is protected !!