January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Meya Mabula Mwanza apingwa

Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula

Spread the love

WAGOMBEA 10 kati ya 20 walioshindwa kwenye kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Jimbo la Nyamagana Jijini Mwanza, wameandika waraka mzito wa kupinga matokeo, yaliyompa ushindi Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Wagombea hao wameandika waraka unaolalamikia matokeo ya uchaguzi huokwamba haukufanyika kwa haki na huru kutokana na kutawaliwa na vitendo vya rushwa vilivyokuwa vikifanywa na meya huyo.

Waraka huo ulioandikwa na wagombea hao umetumwa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdurlahiman Kinana na nakala yake kutumwa kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Phillip Mangula, Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mwanza, Dk. Anthony Diallo, Katibu wa Mkoa, Miraji Mataturu na Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo.

Wagombea hao ni kati ya wanachama 20 wa CCM walijitokeza kuingia katika kinyang’anyiro hicho akiwamo, Mabula ambaye alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 3,553 akifuatiwa na Joseph Kahungwa, kura 3,647 na Raphael Shilatu (kura 864).

Waraka huo ambao ulioandikwa Agosti 2, mwaka huu na kusainiwa na wagombea hao, unaeleza uchaguzi huo wa kura za maoni katika jimbo hilo, uligubikwa na vitendo vya rushwa, ulaghai, dhuluma na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za uchaguzi.

Hata hivyo malalamiko hayo yameelekezwa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Elias Mpanda na Mabula ( Diwani wa Kata ya Mkolani), aliyemaliza muda wake Julai 8, mwaka huu.

Waraka huo umeandikwa na wagombea 10 kama yanavyosomeka hapo ni Stephen Deya, Robert Masunya, Raphael Shillatu, Joseph Kahungwa, Tumaini Lusenga, Wisandara Muhindi, Komanya Kitwala, Dede Petro, Aviasi Said na Tausi Halili..

Pia wagombea hao wanadai na kumtuhumu Katibu huyo wa CCM wa Nyamagana kwamba alitumia lugha kali na vitisho vilivyowanyima wao fursa na uhuru wa kujieleza kwa wapiga kura na kumpatia muda mwingi wa kujieleza.

Wanadaiwa kuwa baadhi ya wapiga kura walikutwa na kadi bandia ambazo walizikabidhiwa kwa katibu huyo ambaye hata hivyo inadaiwa hakuchukua hatua zozote dhidi ya wahusika.

Kwa mujibu wa wagombea hao, madaftari mengi kwenye matawi yalikuwa na majina ya wanachama wapya pekee, huku wa zamini majina yao yakiwa hayaonekani ,hali iliyosababisha wanachama wa muda mrefu kupinga uchaguzi huo katika baadhi ya vituo baada ya kunyimwa fursa na haki ya kupiga kura.

Matawi yaliyokuwa na tatizo hilo ni Maswa Magharibi, Isagenghe, Unguja, Ndofe, Nyamagana, Mwananchi – Tandabui na Nyakabungo, wengi wa wanachama wakiwamo wajumbe wa mashina ( mabalozi), wenyeviti wa mtaa na baadhi ya wagombea udiwani majina yao hayakuonekana kwenye vitabu, hivyo kunyimwa fursa ya kupiga kura.

“Vituo viwili vilivyorudiwa uchaguzi vilifungwa mapema, ambavyo ni Isagenghe kilichofungwa saa 8:00 mchana na Maswa Magharibi kilichofungwa saa 7:30 mchana.Licha ya kuridiwa kwa uvhaguzi,hatukishirikishwa,”

“Uchaguzi katika matawi ya Isagenghe na Maswa Magharibi uliahirishwa na kisha kufanyika siku iliyofuata Jumapili Agosti 2/8/2015 bila wagombea kupewa taarifa na hii imefanyika ili kutoa mwanya kupigwa kwa kura isivyo halali bila mawakala wa wagombea kuwapo vituoni.

“Tumeshuhudia watu wanakuja kupiga kura wakiwa na maelekezo ya kumpigia mgombea ndugu Mabula kutoka kwa mwanachama aliyekiri kuwa ni mtu wa Mabula,” inaeleza sehemu ya waraka huo ( nakala yake tunayo)

Malalamiko mengine yanaeleza kwamba lilikuwapo kundi la vijana wenye umri wa chini ya miaka 14 walioandaliwa kumpigia kura Mabula kwa kutumia kadi za CCM kutoka jimbo jirani la Ilemela.

Inadaiwa katika warka huo kuwa, mmoja wa vijana hao amekiri kumpigia kura Mabula kwa kadi hiyo ambyo imetumika zaidi ya mara moja katika kituo kile kile cha Isagenghe. Kadi hiyo ni namba AF 5590765 iliyotolewa tarehe 25/10/200.

Kuhusu rushwa, wanadai wana ushahidi wa kuthibitisha jinsi Mabula alivyogawa fedha kwa vijana 30 ili wampigie kura ya maoni na baadhi yao waliruhusiwa kupiga kura bila kuwa na kadi za chama,pia alitumia gari T.151 DAY aina ya Noah,kugawa rushwa kwa wapiga kura, iliyopewa jina la gari la BOT.

“Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye ni Katibu wa Wilaya (Mpanda) ameonyesha upendeleo kwa ndugu Mabula tangu kipindi cha kampeni na upigaji wa kura za maoni kwani alionekana kupewa upendeleo wa muda wa kutosha kujinadi kuliko mgombea yeyote.

“Kwa misingi hiyo, hatukubaliani na matokeo hayo na hatuungi mkono juhudi zozote za kumpitisha Mabula aliyeonekana kuhujumu maslahi mapana ya chama na kuharibu mshikamano wa wagombea wenzie na wanachama kwa ujumla.

“Ombi letu, tunaomba busara za chama zitumike ili kukomboa jimbo letu kutoka kwa wapinzani kwa kupata mgombea safi asiyekuwa na wasifu wenye madoa, anayekubalika ndani na nje ya chama,” wanaeleza wagombea hao katika waraka huo.

Juhudi za kumpata Mabula ili kuzungumzia sakata hilo, hazikuzaa matunda baada ya gazeti hili kumpigia simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa na mara nyingine haikupatikana.

Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Elias Mpanda, juhudi za kumpata kiongozi huyo kujibu malalamiko hayo licha ya mwandishi wa habari hizi kwenda ofisini kwake hakumkuta hata alipopigiwa simu yake ya mkononi haikuwa hewani.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu, alipoulizwa amekiri kupokea malalamiko ya wagombea hao wanaopinga matokeo ya kura ya maoni ya ubunge katika Jimbo la Nyamagana na kuongeza kuwa karibu matokeo katika majimbo yote ya mkoa wa Mwanza yamelalamikiwa.

“Malalamiko hayo si Nyamagana pekee, kuna, Ilemela, Magu na Kwimba yote yanalalamikiwa,Watu wanajenga dhana kuwa wanaposhindwa wanalalamika kuwa hawakutendewa haki,” amesema Mtaturu.

Mtaturu amesema ofisi yake haiwezi kuzuia mamlaka ya juu ya chama hicho na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendelea na mchakato wa kupitia na kuthibitisha majina ya wagombea ubunge hadi hapo itakapojiridhisha kuwa malalamiko hayo ni kweli.

error: Content is protected !!