August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Meya Kinondoni aneemesha wafanyabiashara

Spread the love

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imewapa wafanyabiashara wapatao 100 eneo la kufanyia biashara zao katika Soko la Mawasiliano (Sinza), anaandika Happiness Lidwino.

Kwenye soko hilo, wafanyabiashara hao hawatalipa ushuri kwa mwezi mmoja na kisha watatakiwa kulipa.

Boniphace Jacob, Meya wa Manispaa hiyo leo amesema, awali alifanya ziara katika maeneo hayo na kuzungumza na wafanyabiashara ambapo aliwataka kutofanya biashara zao kwenye eneo la Ubungo na badala yake kuhamia Mawasiliano.

“Soko hili ni kwa ajili yenu nyie wamachinga, mama lishe kila mwenye biashara aangalie kunakomfaa na kufanya biashara, kila mtu atapewa kitambulisho kutoka manispaa kimtambulishe eneo lake husika,”amesema.

Amesema, aliona si busara kuwaondoa wafanyabiashara hao bila kuwa na maeneo ya kwenda kufanya biashara zao.

“Niliomba wiki mbili kamati ya ulinzi na usalama ya kinondoni msivunjiwe hadi hapo nitakapowatafutia eneo la kufanya biashara zenu, ni jukumu langu kujua mtakwenda wapi. Kuanzia leo, atakayekuwa Ubungo asinisumbue, watu wangu wako salama mawasiliano,” amesema.

Na kwamba, hatarajii kuona Jeshi la Polisi au mgambo wanawasumbua wafanyabiashara hao huku akiwaomba kuacha njia kwa wanunuzi watakaofika sokoni hapo.

“Hakuna atakayekosa eneo la kufanyia biashara hapa, kila mtu atapata wauza mabegi ule uzio upendeze kwa kutundika mabegi na wauza nguo pia, lakini pia msilipe ushuru kwa mwezi mmoja baada ya mwezi mmoja ndiyo mtalipa,” amesema.

Meya huyo amesema, wafanyabiashara ambao tayari wamepanga biashara zao wasibugudhiwe, waliopewa na kutofanya biashara wapewe watu wengine wafanye.

Baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakiwahi nafasi katika eneo hilo, walilalamika kwa wengine kutopata kwani tayari eneo limeonekana kuwa dogo.

Husna Khamis na Amida Juma ni miongoni mwa wafanyabiashara ambao wamesema, wana wasiwasi na maeneo hayo kutopata kwani waliowahi maeneo hayo asilimia kubwa si wafanyabiashara waliopaswa kuondoka Ubungo.

“Mimi sijapata eneo unavyoniona hapa, kila ninapoangalia naona majani watu wamewahi, ingawa Meya ametuambia tuweke biashara kama eneo halina mtu, ukienda ndani wanakuambi ulipe sh 140,000 ndiyo upate,” amesema Juma.

Awali Jacob alisema, maeneo hayo yamegaiwa bure huku akisisitiza mtu atakayeuza atachukuliwa hatua pamoja na kunyang’anywa eneo husika na kupewa mtu mwingine.

error: Content is protected !!