August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Meya Jacob ataka Chadema kuacha ‘ukondoo’

Boniface Jacob, Meya wa Manispaa ya Ubungo

Spread the love

BONIFACE Jacob, Meya wa Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ubungo, amewataka viongozi na wanachama wa chama chake kuacha kusubiri huruma ya kuruhusiwa kufanya siasa kutoka kwa chama tawala, anaandika Mwandishi Wetu.

Jacob ameyasema hayo ikiwa ni muda mfupi baada ya kuswekwa rumande kwa masaa 48 kwa amri ya Kisare Makori Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, kwa madai ya kutumia ofisi za manispaa kwa shughuli za chama chake – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Meya huyo anayeongoza manispaa ya Ubungo yenye majimbo ya Kibamba na Ubungo, alituhumiwa kuwakaribisha ofisi za halmashauri viongozi wa Chadema Kanda ya Pwani, wakiongozwa na Frederick Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania kwa lengo la kufanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo.

Baada ya kumaliza masaa 48 akiwa katika kituo cha polisi cha Mbezi – kwa Yusufu, Jacob amesema “Kwenu wanachadema wenzangu, kama kuna wanachadema wanategemea huruma za wana CCM (Chama Cha Mapinduzi) kufanya siasa, waache siasa.

Sababu kwa kufanya hivyo, itakuwa ni sawa na kumuomba Sheikh (kiongozi wa kiislamu) akuchinjie nguruwe ili usile nyama haramu.”

Maneno haya ya Jacob yametafsiriwa kama ni kuwataka wanachama wa chama hicho na viongozi kuongeza ari ya kukijenga chama hicho kote nchini bila kujali vikwazo na vitisho vya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.

Viongozi wa Chadema wamekuwa katika wakati mgumu wa kufanya shughuli za kisiasa tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, kwani mikutano ya hadhara na hata vikao vya ndani vimekuwa vikikatazwa na kuingiliwa na Jeshi la Polisi mara kwa mara.

Pia Rais John Magufuli ametoa amri ya kupiga marufuku mikutano ya hadhara kwa viongozi wa vyama vya siasa wasiokuwa wabunge au madiwani na akiamuru wenyeviti, madiwani, na wabunge wafanye mikutano hiyo katika majimbo wanayoyaongoza tu. .

 

error: Content is protected !!