October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Meya Jacob agonga mwamba kuingia ofisini, barua zamiminika kwa DED

Ofisi za Manispaa ya Ubungo

Spread the love

BONIFACE Jacob, Meya wa Manispaa wa Ubungo jijini Dar es Salaam leo Jumatatu tarehe 4 Mei 2020 ameshindwa kuingia ofisini kuendelea na majukumu yake ya kila siku. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua hiyo inatokana na juzi Jumamosi tarehe 2 Mei 2020 kuwapo kwa taarifa zenye utata kwamba Jacob amevuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Taarifa hizo zilipata uzito baada ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Betrice Dominick kumwandikia barua Jacob ya kumtaka akabidhi mali na vifaa vyote alivyokuwa akitumia.

Leo Jumatatu, Mwanahalisionline limefika katika ofisi za Manispaa ya Ubungo zilizopo Ruguluni kuangazia kama Jacob ataingia ofisini kama alivyoueleza umma jana Jumapili kwamba yeye bado ni Meya wa Ubungo.

Hata hivyo, Jacob ambaye pia ni Diwani wa Ubungo amejikuta akigonga mwamba kuingia ofisini kwa kile alichoeleza amepokea rasmi barua iliyoandikwa na mkurugenzi hivyo anafanya utaratibu wa kuijibu.

Mbali na Jacob kuandika barua, kuna barua tatu tofauti zimeandikwa kwenda kwa mkurugenzi huyo kuhusu suala hilo ambazo ni ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, katibu wa Chadema kata ya Ubungo, Ezekiel Tulyanje na ya Ashery Mlahagwa.

Barua ya Mnyika imewasilishwa leo kwa mkurugenzi inayozungumzia kuwa Jacob bado ni mwanachama wa chama hicho, diwani na meya na kumtaka mkurugenzi huyo kutengua uamuzi aliokwisha ufanya.

Akizungumza barua yake, Mlahagwa amesema jina lake lilitumika visivyo kuandika barua iliyokwenda kwa mkurugenzi kumweleza wamemvua uanachama Jacob wakati yeye si kiongozi.

“Mimi sikuandika barua hiyo wala mimi si kiongozi, nimemwandikia barua mkurugenzi ambayo nimeiwasilisha leoleo kumweleza mimi sihusiki na mimi siyo katibu wa Chadema bali nilikuwa na nafasi hiyo mwaka 2018,” amesema

Kwa upande wake, Tulyanje amesemam, “nimemwandikia barua mkurugenzi kumweleza mimi kama katibu wa Chadema kata ya ubungo, hakuna kikao chochote kilichokaa cha kumjadili Jacob na wala sisi hatuna mgogoro wowote na Meya Jacob.”

“Tumemwomba mkurugenzi atusaidie kumjua huyo aliyeandika barua ni nani, lakini vyombo vya dola navyo vitusaidie kujua huyo aliyeghushi ni nani. Lakini mkurugenzi kwa nafasi yake alipaswa kujiridhisha kwanza kabla ya kuchukua uamuzi huo,” amesema Tulyanje

Mwanahalisionline limefika ofisini kwa Mkurugenzi wa Ubungo, Betrice kuzungumza naye kuhusu hiki kinachoendelea lakini hakuwepo na alipopigiwa simu alitaka atumiwe ujumbe mfupi wa maandishi, hata alipotumiwa kutaka kujua kipi kinaendelea alijibu, “nipo kwenye uboreshaji.”

Uboreshaji anaozungumzia ni wa daftari la kudumu la wapiga kura linaloendelea jijini Dar es Salaam.

error: Content is protected !!