Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Meya Isaya akalia kuti kavu
Habari za SiasaTangulizi

Meya Isaya akalia kuti kavu

Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam
Spread the love

MEYA wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita (Chadema), amekalia kuti, kufuatia hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), “kumsukia zengwe,” kutaka kumng’oa katika nafasi yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Meya Isaya ambaye alipatikana baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa 25 Oktoba 2015, ametuhumiwa na madiwani wa CCM kwa matumizi mabaya ya madaraka.

Hata hivyo, kinachoitwa na chama hicho kuwa matumizi mabaya ya madaraka, kimeelezwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa siyo kingine, bali ni ubinafsi na uroho wa madaraka.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya jiji la Dar es Salaam, Meya Isaya anadaiwa kutotumia kiasi cha Sh. 5.8 bilioni, zilizotokana na mauzo ya hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), ambalo lilikuwa mali ya jiji.

Shirika la UDA, ambalo mwaka 1983 Msajili wa Hazina alitoa asilimia 51 ya hisa kwa Halmashauri ya Jiji, huku serikali kuu ikibakiwa na asilimia 49, liliuzwa kinyemela na Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam.

Masaburi alikabidhi UDA kinyemela kwa kampuni ya Simon Group Limited, bila kushirikisha baraza la madiwani la jiji na msajili wa hazina.

Mkutano wake uliyopitisha mauzo, ulihudhuriwa na watu wanne tu – Dk. Didas Masaburi mwenyewe ambaye alikuwa mwenyekiti, mkurugenzi wa Simon, Robert Kisena ambaye alikuwa katibu na Mwanasheria wa jiji, Isaac Nassor Tasinga na kaimu mkurugenzi wa jiji, Phillip Mwakyusa.

Kwenye mkutano huo, ndipo Masaburi alitangaza kampuni ya Simon kuwa “imetimiza masharti yote ya mkataba wa kupewa hisa, mali na uendeshaji wa UDA.”

Taarifa ya serikali ya 3 Agosti 2011 kwenda Kamati ya Bunge ya Miundombinu inasema mkutano huo ulikuwa batili kwa kuwa ulikiuka katiba ya UDA kifungu cha 45 kutokana na kutotimia kwa akidi na kukosekana kwa msajili wa hazina.

Serikali inasema kikao hicho hakikuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi na maazimio yote yaliyofikiwa yalikuwa batili.

Kufuatia utata huo, ndipo baraza la jiji lilipitisha kwa kauli moja, kuzuia matumizi ya fedha hizo; na kutaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na uhalali wa uuzaji wa shirika hilo.

Lakini baadaye – kwa shinikizo la mkurugenzi wa jiji aliyepo sasa, Sipora Liana, baraza la madiwani lenye madiwani wengi wa CCM, lilibatilisha maamuzi hayo kwa kuamuru fedha hizo kutumika.

“Kwa tuhuma hii pekee, inathibitisha kuwa CCM, hakipambanani na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Hii ni fedheha kubwa kwa chama na taifa. Kwamba mtu ambaye alisimamia maamuzi ya baraza kwa kutaka kufanyika uchunguzi wa uuzaji wa shirika, leo anaonekana mbaya. Nakuambia, tutaadhibiwa na wananchi, ” ameeleza mmoja wa madiwani wa jiji ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

Aidha, Isaya anatuhumiwa kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kupendelea baadhi ya mameya kuingia katika kamati za fedha.

Kwa mujibu wa kanuni za halmashauri ya jiji, mameya wote wanaotokana na manispaa zinazounda jiji la Dar es Salaam, ni wajumbe wa kamati za fedha.

Manispaa zinazounda jiji, ni Halmashauri ya Manispaa ya Ilala; Kinondoni, Ubungo, Temeke na Kigamboni.

Madai mengine, ni matumizi mabaya ya gari umma kwa kulisababishia kupata ajali, jambo ambalo meya amekuwa akijibu kwamba yeye siyo dereva wa gari hilo.

Kamati ya kuchunguza tuhuma hizo, inadaiwa imeundwa na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Tayari Sipora ameitisha kikao cha kumjadili meya kesho Alhamisi, tarehe 9 Januari 2020, kitakachofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee, kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Kwenye barua ya wito kwa wajumbe wa kikao hicho, Sipora anasema, miongoni mwa ajenda tatu za kikao hicho ni pamoja na kupokea taarifa ya timu ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Meya Isaya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!