July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Meya Ilala kuvuna mamilioni

Spread the love

CHARLES Kuyeko, Meya wa Manispaa ya Ilala anasubiri kuvuna zaidi ya Sh. 20 milioni ikiwa ni fidia baada ya kushinda kesi iliyofunguliwa na mpinzani wake Sabir Malilo, anaandika Happyness Lidwino.

Ni baada ya Mahakama ya Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana kumpa ushindi katika kesi yake ya kikatiba ya kupinga matokeo ya udiwani iliyofunguliwa na mpinzani wake Malilo.

Uchaguzi uliompa ushindi Kuyeko ni ule uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana kwenye Kata ya Bonyokwa-Tabata, Dar es Salaam.

Malilo alisimama kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku Kuyeko akikiwakilisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kuyeko amesema, pesa hizo zinahusu gharama za mawakili wake wawili waliosimamia kesi yake ambao na kuwa, zipo gharama zingine ikiwemo usafiri wa yeye na familia yake kwenda mahakamani, chakula pamoja na muda aliopoteza kufuatilia kesi hiyo na kwamba, anatarajia kupeleka hesabu kamili mahakamani baada ya kukutana na mawakili wake.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Kuyeko amesema, mahakama hiyo iliifuta kesi ya kikatiba iliyokuwa imefunguliwa na Malilo ikiwa ni baada ya kujiridhisha na utetezi wake ambapo ilibainika kutokuwepo kwa mashiko.

Amesema, uamuzi wa kufutwa kwa kesi hiyo ulitolewa na Cyprian Mkeha ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi na kuwa, mahakama imeamua kufuta kesi hiyo baada ya kupata utetezi wa upande wa mshitakiwa uliotolewa na Wakili John Malya na kutosheleza.

Kuyeko amesema, katika kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2015 mlalamikaji ambaye ni Malilo alipinga matokeo ya ushindi wake kwa madai ya kumwibia kura katika uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana.

Akitaja mashitaka mengine Kuyeko amesema, Malilo pia alimtuhumu kuwa siku ya uchaguzi alimkuta akizungumza na msimamizi wa kituo cha Kifulu, pia alidai uchaguzi ulikuwa na fujo.

“Hayo ni baadhi ya mashitaka ambayo alinishitaki, baada ya mahakama kuyapitia kwa makini ilibaini kuwa ndani yake kulikuwa na uongo mwingi pia mshitaki hakutoa ushahidi wala ufafanuzi wa kutosha kuthibitisha mashitaka yake.

“Pia kwa hali ya kawaida mimi wa chama pinzani ni ngumu kuiba kura kiliko yeye chama wa tawala,” amesema Kuyeko.

Hata hivyo, Kuyeko ameeleza kuridhishwa na uamuzi wa mahakama na hivyo ametoa wito kwa mahakama zingine kutenda haki bila upendeleo.

error: Content is protected !!