August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Meya Ilala aendelea kutekeleza ahadi

Charles Kuyeko, Meya wa Manispaa ya Ilala

Spread the love

CHARLES Kuyeko, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala ambaye pia ni Diwani wa kata ya Bonyokwa, amesema tayari ametekeleza ahadi ya alizotoa wakati akiwania uongozi wa kata hiyo Oktoba mwaka jana, ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu achaguliwe, anaandika Pendo Omary.

Kuyeko amesema ahadi hizo ni vipaumbele vya ilani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vinavyolenga kuwawezesha wananchi kufikia maendeleo endelevu.

Miradi ya maendeleo ambayo imefanikishwa na diwani huyo mpaka sasa ni ujenzi wa madarasa matano katika Shule ya Msingi Bonyokwa ambao umegharimu Sh. 85,000,000/= (milioni themanini na tano) pamoja na kutatua kero ya madawati katika shule zote zilizo katika kata ya Bonyokwa.

Kuyeko amesema kwamba kwa sasa hakuna mwanafunzi yoyote anayekaa chini katika shule iliyopo kata ya Bonyokwa.

“Katika kipindi cha mwaka mmoja, nimefanikisha uchimbaji wa visima vitatu vya maji kupitia ufadhili wa African Muslims Agency, visima hivyo vimechimbwa katika maeneo ya shule ya msingi Bonyokwa, shule ya msingi Kifuru na mtaa wa Kisiwani,” amesema Kuyeko.

Kuyeko pia amesema amefanikiwa kutatua kero ya muda mrefu iliyokuwa ikijitokeza hususan kipindi cha mvua ambapo amejenga daraja la linalounganisha kata hiyo na kata jirani ya Kinyerezi na hivyo kuifanya Bonyokwa kutokuwa kisiwa tena wakati wa mvua.

“Katika kutatua kero ya miundombinu ya barabara, nimefanikisha ujenzi wa barabara ya lami ya Segerea-Bonyokwa ambapo sasa ujenzi unaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Machi 2017,” ameeleza.

Kuyeko amesema kuwa kwa sasa anashughulikia ujenzi wa ofisi za mitaa, ofisi za kata, vituo vya afya, na vyoo katika shule za msingi ambapo ameahidi kukamilisha miradi hiyo pia.

Ametoa wito kwa viongozi wa serikali na wananchi kumuunga mkono na kumpa ushirikiano bila kujali itikadi za vyama vyao.

error: Content is protected !!