September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Meya, Ded Mwanza watifuana

Spread the love
MGOGORO umeibuka kati ya James Bwire, Meya wa Jiji la Mwanza na Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji hilo kuhusu madai ya kutengenezwa madawati 8500 yanayodaiwa yapo chini ya kiwango, anaandikaMoses Mseti.
Meya Bwire, kwa muda mrefu amekuwa kwenye mgogoro na Adam Mgoyi, aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji hilo. Mgoyi kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro. 
Mvutano huo umeibuka baada ya Bwire kunukuliwa na gazeti moja la kila siku kwamba, madawati yaliyotengenezwa na halmashauri hiyo yapo chini ya kiwango na kwamba hayafai.
Hata hivyo, baada ya madai hayo, Kibamba ameibuka na kudai kuwa, maelezo yaliyotolewa katika gazeti hilo (yakimnukuu Bwire) kwamba madawati yapo chini ya kiwango sio kweli.
Kibamba jana amesema, baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa madiwani wakidai kuwa wameigizwa mkenge, baadhi ya madiwani na wakuu wa idara walikwenda kuyaangalia madawati hayo.
“Madiwani na baadhi ya watu wanasema kwamba mbao zilizotengeneza madawati haya ni soft wood (mbao nyepesi) na sio hard wood (mbao ngumu), sasa leo (juzi) waliamua kwenda `site` kuangalia na kujihakikishia kama maelezo hayo ni ya kweli,” amesema Kibamba.
Kibamba amesema, baada ya madiwani hao kufika eneo husika yanakotengenezwa madawati hayo, waliamua kuchukua baadhi ya madawati na kuyapelekea kwa wataalamu wa misitu ambao anadai walijiridhisha ni imara.
Kibamba ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amesema kuwa uongozi wa jiji hilo upo makini katika kufuatilia kazi ya utengenezaji wa madawati hayo na kwamba, hatakubali madawati yakitengenezwa chini ya kiwango.
“Mpaka sasa hivi tumetengeneza madawati 8500, yaliyobaki ni 900 na hiyo yote ni kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa 2000 katika shule zetu za umma na tumeamua kuanza kutengeneza madarasa kwanza,” amesema Kibamba.
Hata hivyo, mtandao huu ulipomtafuta meya ofisini kwake kuzungumzia suala hilo, alidai kwamba hana cha kuzungumza na kuwa, atafutwe Elirehema Kaaya, Ofisa Mahusiano wa Jiji.
Kaaya alipoulizwa alisema, hawezi kuzungumza kwa kuwa bosi wake (mkurugenzi) tayari amelizungumzia suala hilo.
“Mimi sikatai kuzungumza ila kwa sababu bosi wangu tayari kazungumza na kiitifaki, akizungumza bosi wako wewe (yeye) hauwezi kuzungumza chochote na mimi ni mtaalamu wa itifaki,” amesema Kaaya.
Mmoja wa watumishi wa halmashauri hiyo, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, amesema kuwa anamshangaa meya huyo, kuibuka dakika hizi za mwisho kudai madawati yapo chini ya kiwango.
“Yeye kipindi madawati haya yanatengenezwa, alikuwepo na huyu mkurugenzi hakuwepo, kwanini hakuyasema hayo anayoyasema tangu zamani  kabla hayajaanza kutengenezwa labda kuna kitu hapo ,” amesema mtumishi huyo.
error: Content is protected !!