December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mexime, kiboko ya makocha wageni

Wachezaji wa Mtibwa Sugar wakimdhibiti kiungo wa Azam, Frank Domayo katika mchezo wa robo fainali ya Mapinduzi Cup

Spread the love

JINA la Mecky Mexime huwezi kulikosa kwenye mafaili ya makocha wa kigeni waliokuja nchini kuzifundisha timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, anaandika Erasto Stanslaus.

Unajua sababu ya jina hilo kuwa kwenye mafaili ya wageni? Sababu kubwa ni matokeo wanayopata makocha hao wanapokutana na vijana wa Mexime uwanjani.

Mexime anayeinoa timu ya Mtibwa Sugar ndiye kocha pekee wa Tanzania anayewavuruga makocha wa kigeni kwa kuzibania timu zao wanazozifundisha kila wanapokutana nazo kwenye michezo ya ligi na michuano mingine.

Katika msimu huu, Kocha wa kwanza kukutana na kibano cha Mexime, ni Mbrazil Marcio Maximo wa Yanga alikubali kichapo cha mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Septemba 20, 2014 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Patrick Phiri wa Simba naye alionja chungu baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 kutoka kwa Mtibwa katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Novemba 1, 2014 lakini walipocheza Chamanzi katika mchezo wa kirafiki walikubali kichapo cha mabao 4-0.

Naye Jackson Mayanja wa Kagera Sugar aliambulia sare ya bao 1-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Novemba 8, 2014.

Mexime alimuondosha Joseph Omog wa Azam katika michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuitoa Azam kwa mikwaju ya penalti 7-6 katika mchezo wa robo fainali uliochezwa Januari 8, 2015 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika dakika za kawaida.

Baada ya Simba kumtimua Phiri na nafasi yake kuchukuliwa na Goran Kopunovic lakini Mexime hakusita kumkaribisha Mserbia huyo kwa kichapo cha bao 1-0 katika mchezo wa makundi wa Kombe la Mapinduzi uliochezwa Januari mosi, 2015.

Mexime anaongoza Ligi Kuu Bara baada ya kucheza michezo nane na kukusanya pointi 16, akifuatiwa na Yanga na Azam wenye pointi 14 kila moja.

error: Content is protected !!