September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Membe yametimia, Makamba amkana

Spread the love

BERNARD Membe, Waziri wa Mambo ya Nje Mstaafu, ameandikiwa barua ya wito, kwenda kuhojiwa kwenye Kikao cha Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa na Membe leo tarehe 4 Februari 2020, kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Katika andiko hilo, Membe amesema kikao hicho kitafanyika tarehe 6 Februari mwaka huu, kuanzia saa tatu asubuhi.

“Hatimaye, jana jioni nimepokea barua ya kuitwa kwenye kikao cha Kamati ndogo ya Udhibiti na Nidhamu Jijini Dodoma. Kikao kitafanyika tarehe 6/02/2020 saa 3 Asubuhi kwenye jengo la White House. Nitahudhuria bila kukosa na bila kuchelewa! Stay tuned!,” ameandika Membe katika ukurasa wake wa Twitter.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Halmashauri Kuu ya CCM, mwishoni mwa mwaka jana, kuagiza Membe pamoja na Makatibu Wakuu Wastaafu wa CCM, Mzee Yusuph Makamba na Abdulrahman Kinana, kuhojiwa kifuatia tuhuma zinazowakabili.

Membe pamoja na makatibu hao wastaafu wa CCM, wanatuhumiwa kwa utovu wa nidhamu.

MwanaHALISI ONLINE ilimtafuta Mzee Makamba kwa ajili ya kufahamu kama na yeye amepewa barua ya wito kwa ajili ya kwenda kuhojiwa kufuatia tuhuma hizo, na kueleza kwamba hajapata barua hiyo.

“Wanaohusika sio mimi,  waulize hao. Kama wamemuandikia Membe, Membe sio mwenzangu kila mtu na lake. Kama Membe amepata barua andika Membe amepata,” amesema Mzee Makamba na kuongeza:

“Mimi nasema hivi, waulize walioandika barua, mmemuandikia Mzee Makamba?  Waulize wao kwanza kwamba mmeamuandikia, halafu uniulize mimi.”

error: Content is protected !!