Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Membe: Sina sababu ya kuomba radhi
Habari za SiasaTangulizi

Membe: Sina sababu ya kuomba radhi

Spread the love

WAZIRI wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa wa zamani wa Tanzania, Bernard Membe amesema, hana sababu ya kumuomba radhi Rais John Magufuli, wala
Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, “mtu anaomba radhi kama amemkosea mtu au watu,” na kwamba yeye hajamkosea yeyote na hivyo, hana sababu ya kuomba radhi.

Kwa mujibu wa Membe, mtu ambaye anaomba radhi wakati akiwa hana makosa, ni “mwoga na asiyejiamini.”

Membe ametoa kauli hiyo jana Jumamosi, 6 Juni 2020, ikiwa ni siku mbili tangu aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kujitokeza hadharani kumwomba msamaha Rais Magufuli na chama chake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Alhamisi iliyopita, Kinana alisema, anamwomba Rais Magufuli amsamehe kutokana na mazungumzo kati yake na baadhi ya makada wengine wa CCM, ambayo yalifanyika kwa njia ya simu na ambayo yalikuwa na nia ovu dhidi ya kiongozi huyo na chama hicho tawala.

Kinana amechukua hatua hiyo ya kuomba radhi, katika kipindi ambacho yuko chini ya “uangalizi wa miezi 18,” ambapo katika kipindi hicho, hataruhusiwa kugombea uongozi wowote.

Mwanasiasa huyo mashuhuri nchini, alipewa adhabu hiyo, inayotafsiriwa na wachambuzi wa msuala ya kisiasa, kuwa sawa na “kufungwa spidi gavana,” na Kamati Kuu (CC) ya CCM, tarehe 28 Februari 2020.

Wakati Kinana akipewa adhabu ya kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi 18, Kamati Kuu ilimsamehe Yusuf Makamba, katibu mkuu wa zamani wa chama hicho.

Katika mkutano huo, Membe alimfukuzwa uanachama kwa kile kilichoelezwa na chama hicho, “kuwa na mienendo isiyoridhisha.”

Membe anasubiri hatima yake mbele ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, ambako chombo hicho, kinaweza kuidhinisha adhabu ya Kamati Kuu ya kumfukuza,
kumsamehe; na au kumbadilishia adhabu.

Kinana amekuwa kada wa nne kumwomba radhi Rais Magufuli kutokana na mazungumzo hayo yaliyotikisa medani za siasa nchini mwaka 2019 kusambaa katika mitandao ya kijamii.

Alikuwa akizungumzia kuporomoka kwa chama hicho kisiasa na utendaji wa uenyekiti na urais wa Magufuli.

Akionekana kujutia maneno yake, Kinana alisema, wakati anashughulikia suala lake (ambalo hakulitaja) alitumia njia zisizokuwa sahihi.

Alisema, “…najua nilikereka na vitu fulani na nikahuzunika na kukaairika katika kushughulika na suaa lile na kusema mambo ambayo hayakuwa mazuri kwa Rais na mwenyekiti wangu.”

Aliongeza, “baada ya kutafakari nimeona niombe radhi kwa kusema ndugu mwenyekiti nimekukwaza, nimekuhuzunisha, nikuombe radhi kwa yale niliyoyasema.

“Katika maisha ni uungwana kukaa na kutafakari na bila shaka atanisikia na atanisamehe.”

Wengine watatu waliosamehewa na Rais Magufuli baada ya kuomba radhi na NEC kutoa msamaha, tarehe 13 Desemba 2019, ni pamoja na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba.

Nape yeye alikwenda Ikulu ya Dar es Salaam kumwomba radhi huku Januari na Ngeleja Rais Magufuli akieleza walimwomna ila haikuwa hadharani kama ilivyokuwa kwa Nape na sasa Kinana.

Kinana, Makamba na Membe walikutwa na kadhia hiyo baada ya kuwa wamehojiwa na kamati ya maadili iliyokuwa iliongozwa na makamu mwenyekiti wa CCM- Bada, Philip Mangula.

Msingi wa mahojiano hayo ya sauti zao, yalitanguliwa na waraka wa Kinana na Makamba wa Julai 14 mwaka 2019 kwenda kwa Katibu wa Baraza la Wazee la CCM, Pius Msekwa.

Katika waraka huo, viongozi hao walidai uongozi huo hauwalindi wao dhidi ya mtu ambaye alikuwa akiwadhalilisha na walimwelezea analindwa na mtu mwenye mamlaka.

Akiandika jana Jumamosi tarehe 7 Juni 2020, kupitia ukurasa wake wa twitter, Membe ambaye ni mwanadiplomasia mashuhuri na mbunge wa zamani wa Mtama mkoani Lindi, alisema kuwa hawezi kufanya yale aliyofanya Kinana.

Alisema, “tangu Mheshimiwa Kinana aombe radhi, nimepokea messages (ujumbe) nyingi sana za kutaka kujua msimamo wangu.

“Mtu anaomba radhi kama; i) amemkosea mtu au watu. ii) mtu huyo ni mhalifu.iii) mtu huyo ni mwoga na hajiamini au iv) amekuwa “blackmailed.” Sihusiki na hayo yote na hivyo SITAOMBA RADHI,” alisisitiza.

Msimamo huo wa Membe umeibua mjadala kwa kila mmoja kuzungumza lake. Wapo wanampongeza na wengine wanamtaka kubadili msimamno wake ili yaishe.

Msimamo wa Membe umeanza kuwavutia baadhi ya watu, huku wengine wakimpendekeza kuwa mgombea urais katika uchaguzi ujao, kwa kile wanachokiita, “mkombozi mpya katika lindi la ukandamizaji.”

1 Comment

  • Mheshimiwa ametoa msimamo wake ambao ni kweli kwa maisha ya mwanadamu anayejitambua ambaye anajua kuwa Binadamu wote ni sawa mbele ya sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

error: Content is protected !!