January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Membe, Pinda ‘wajiengua’ mbio za urais

Waziri Mkuu, Mizeongo Pinda akifurahia jambo na Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe

Spread the love

MIZENGO Pinda na Bernard Membe, tayari wamejiengua katika orodha ya wanaosaka urais kupotia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaandika Saed Kubenea…(endelea).

Ni vigumu kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri, Mizengo Pinda na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kufanikiwa kupenya katika mbio zao za kusaka urais, MwanaHALISI Online limeelezwa.

“Hawawezi kupitishwa na chama chao. Lakini hata wakipita, wawili hawa hawatakuwa na nafasi ya kushinda katika sanduku la kura la jumla,” ameeleza waziri mmoja mwandamizi serikalini.

Matukio mawili makubwa yanatajwa kuwa na athari mbaya sana kwa Pinda na tayari yamesambaratisha moja kwa moja “mradi” wake wa kutaka urais.

Matukio hayo, ni mahakama ya kadhi na kashfa ya ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Escrow.

Kiongozi mmoja wa ngazi ya juu ndani ya CCM amesema, “Pamoja na Pinda kuponyoka kwenye kashfa ya Escrow, lakini tayari amejimaliza kisiasa.”

Anasema, “Pinda amejidhoofisha sana katika sakata la Escrow kwa kuwa wananchi wanajua yule Singasinga walikutana Ikulu kabla ya kukutana na Rais Jakaya Kikwete; na kutoka hapo ndipo alipoamuru kukwapuliwa kwa mabilioni ya shilingi BoT.”

Pinda ni mmoja wa watuhumiwa muhimu katika ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow.

Kwa mujibu wa andishi la Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndullu, makubaliano ya kugawa fedha za umma kwa Harbinder Singh Sethi “yalipata baraka za mkuu wa nchi ambaye ni Rais Jakaya Kikwete na waziri mkuu Pinda.”

Pinda alifahamu kuwapo makubaliano ya kuhamisha fedha, kinga dhidi ya madai au mashitaka baada ya malipo; na kukwepa kulipa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Anatuhumiwa kutotimiza wajibu wake; kutojiridhisha na uhalali wa malipo na kushindwa kumshauri vema Rais Kikwete ambaye siyo mwanasheria, juu ya utata ulioibuka kuhusu kampuni mpya ya Pan African Power Solution (PAP), kumiliki hisa katika IPTL.

Aidha, kiongozi huyo anataja hatua ya Pinda ya kujiingiza katika “Mahakama ya Kadhi,” imezidisha kumomonyoa mpango wake wa kusaka urais.

“Hili la Mahakama ya Kadhi alilotwisha huyu bwana (Pinda) haliwezi kumuacha salama. Ni lazima litamuangusha.”

Hoja ya kuanzishwa Mahakama ya Kadhi nchini, tayari imeibua mvutano mkubwa, hasa baada ya viongozi wa madhehebu ya Kikirsto kupinga kuanzishwa kwa mahakama hiyo.

“Sakata la Mahakama ya Kadhi” lilianzia ndani ya Bunge Maalum la Katiba, pale Pinda alipoahidi viongozi wa madhehebu ya Kiislamu kuwa serikali itaanzisha mahakama hiyo.

Pinda alitoa ahadi hiyo ili kuwalainisha baadhi ya Waislamu waliokuwa wameapa kutopigia kura vifungu vya rasimu vya katiba ikiwa suala la Mahakama ya Kadhi halitaingizwa ndani ya Katiba Mpya.

Naye Membe anatajwa kujiondoa katika mbio hizo za urais kwa kile kinachoitwa, kijiingiza katika “kupigania OIC” na kujiegemeza kwa Rais Jakaya Kikwete.

Membe amekuwa akiliambia Bunge, tangu Agosti 2008, kuwa Jamhuri kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC); ambako kunadaiwa kuwa moja ya vipengele vyake vya katiba, vinadaiwa kutaka nchi kujiegemeza kwenye dini.

“Sakata la OIC” liliibuka kwa mara ya kwanza nchini mwaka 1993, pale uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya Dk. Salmin Amour, ulipoamua kujiunga na jumuiya hiyo.

Hatua ya Zanzibar kujiunga na OIC ilizua mvutano mkubwa miongoni mwa viongozi wa juu wa serikali; jambo ambalo lilisababisha waziri mkuu wa wakati huo, John Malecela na Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba kufutwa kazi.

Mwingine aliyefutwa kazi katika sakala hilo, ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Ahmed Hassan Diria.

“Huyu Membe ameshindwa kusoma alama za nyakati. Amejimaliza katika OIC na sasa anajiegemeza kwa Kikwete kwa lengo la kutaka kuwa rais. Hatafanikiwa,” anasema ofisa mmoja mwandamizi katika idara ya usalama wa taifa.

Amesema, “Kila mmoja anajua kuwa Kikwete hana ubavu wa kumpa mtu urais. Hivyo kujiegemeza naye, ni kupoteza muda.”

error: Content is protected !!