October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Membe atajwa Mkutano mkuu ACT-Wazalendo

Spread the love

JINA la Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje Mstaafu, limetajwa katika Mkutano Mkutano Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, unaoendelea katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Jina hilo limetajwa leo tarehe 14 Machi 2020 na Dk. Azaveli Lwaitama, wakati akizungumzia hoja ya upatikanaji wa mgombea binafsi wa urais.

Dk. Lwaitama amelitaja jina la Membe kipindi ambacho mwanasiasa huyo amefurushwa katika Chama chake cha Mapinduzi (CCM), kwa kosa la utovu wa nidhamu.

Hata hivyo, Membe anadai hatua ya kufukuzwa CCM inatokana na harakati zake, za kutaka kugombea urais kwenye uchaguzi ujao kupitia chama hiko.

Kufuatia sakata hilo, Dk. Lwaitama amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa, kama sheria za nchi zingeruhusu mgombea binafsi, Membe asingehangaika kutafuta fursa ya kugombea Urais wa Tanzania kupitia vyama vya siasa.

Mwanazuoni huyo ameeleza kuwa, kutokuwepo kwa fursa hiyo, kunaweza pelekea Membe kuhangaika katika vyama vingine vya siasa pasina mafanikio, kisha kurejea katika Chama chake cha CCM.

“Bila ya kuwa na nguvu ya umma huwezi kuwa na mgombea huru, kusudi Membe awe na akili nzuri zaidi ya kugombea badala ya kuhangaika huko, baadae kurudi nyumbani,” amesema Dk. Lwaitama.

Wakati huo huo, Dk. Lwaitama ameshauri sheria ya uchaguzi kurekebishwa, ili kuruhusu mgombea binafsi wa urais, kwa kuwa hilo lilikua takwa la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Amesema Mwalimu Nyerere alikufa akipigania nchi kuwa na sheria inayoruhusu mgombea binafsi.

error: Content is protected !!