Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Membe asamehewa, arejeshwa CCM
Habari za SiasaTangulizi

Membe asamehewa, arejeshwa CCM

Spread the love

BAADA ya kusota ‘benchi’ kwa muda wa mwaka mmoja na ushee, Kada aliyejipatia umaarufu kisiasa ndani ya CCM na baadaye ACT Wazalendo, Bernard Membe amewasamehewa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na kurudishiwa uanachama wake.

Mbali na Membe pia kada mwingine Abdalah Maulid Diwani kutoka Zanzibar ambaye pia alikuwa mwakilishi wa jimbo la Jang’ombe naye amesamehewa na kurejeshewa uanachama wake baada ya kufutiwa mwaka 2018. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma… (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo tarehe 31 Machi, 2022, Katibu wa NEC itikadi na uenezi – CCM, Shaka Hamdu Shaka amesema hatua hiyo imekuja baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa CCM kufuatilia mienendo wanachama hao na kuridhishwa.

Amesema kwa mujibu wa matakwa ya kikatiba ibara ya 102 (8), kazi za Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, kazi zake za msingi ni ni kufuatilia mienendo pamoja na taratibu za wanachama wake.

“Mtakumbuka Bernad Membe alikuwa mwanachama wa CCM na baada ya yale yaliyotokea alifutiwa au aliondoshwa nbdani ya CCM.

“Pia yupo Abdalah Maulid Diwani kutoka Zanzibar alikuwa mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe naye mwaka 2018 alifutiwa uanachama wake wa CCM.

“Ninafuraha kuujulisha umma kuwa leo tarehe 31, Machi 2022 katika kukidhi matakwa ya katiba, Halmashauri Kuu ya Taifa CCM imewasamehe na imewarudishia uanachama wao,” amesema.

Amesema kuanzia leo Membe na Diwani ni wanachama wa CCM na taratibu nyingine za kuwapatia kadi zao za uanachama zitafanyika katika maeneo yao kama ambavyo katiba ya imeelekeza.

MSUKOSUKO WA MEMBE CCM

Kabla ya kurejeshewa uanachama leo, Membe ambaye pia ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje alivuliwa uanachama pamoja na madaraka na kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tarehe 28 Februari, 2020.

Mbali na Membe, pia Katibu wakuu wa mstaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipewa onyo na kutokugombea nafasi yoyote ndani ya chama kwa miezi 18.

Hata hivyo, baadaye Kinana alisamehewa sambamba na Katibu Mkuu wa zamani, Yusuf Makamba.

Membe na wenzake walipewa adhabu hizo kupitia maamuzi ya Kikao Cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika wakati huo jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa CCM, Hayati Rais Dk. John Magufuli.

Kabla ya Kikao cha Kamati Kuu (CCM) cha leo, hivi karibu Kamati Kuu hiyo ilifanya kikao ambapo pamoja na mambo mengine ilitoa siku saba kwa Kamati Ndogo ya Nidhamu na Maadili iliyowahoji Kina Kinana, Membe na Makamba kukamilisha taarifa na kuwasilisha kwenye vikao vitakavyofuatia.

Pia walikuwa tayari wameshahojiwa na Kamati hiyo kwa nyakati tofauti ambapo Membe alihojiwa jijini Dodoma na Kinana na Mzee Makamba walihojiwa jijini Dar es Salaam kutokana na tuhuma za makosa ya kimaadili.

Agizo la kuhojiwa Kina Membe, Kinana na Mzee Makamba, lilitolewa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM katika Kikao chake kilichofanyika jijini Mwanza, tarehe 13 Desemba, 2019.

Viongozi hao wastaafu waliingia matatani baada ya sauti zao kusambazwa na baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii wakieleza mambo mbalimbali na madai ya chama kushindwa kuwalinda Makatibu Wakuu hao wastaafu dhidi ya mtu anayejiita mwanaharakati, ambaye alisambaza sauti hizo na akitoa tuhuma dhidi yao.

“Uamuzi huu umekuja baada ya kuwa taarifa zake ndani ya chama zinaonyesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha lakini imeonekana sivyo,” alisema Humphrey Polepole aliyekuwa Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM.

MEMBE NA NANI?

Membe ni mwanasiasa machachari wa Tanzania ambaye amewahi kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Hata hivyo, katika mchakato huo, Membe alipigwa chini na nafasi hiyo kunyakuliwa na Dk. John Magufuli huku akiwaacha solemba Membe na Edward Lowassa ambao ndio makada waliokuwa wakitajwa kwa muda mrefu kuwa vinara wa nafasi hiyo.

Aidha, baada ya Membe kushindwa katika mchakato huo wa kuwani urais, mwaka 2018 alianza kutuhumiwa kujaribu kumzuia rais Magufuli asipewe nafasi ya kugombea tena mwaka 2020.

Licha ya kufungua kesi ya kuchafuliwa jina ya gazetini, Membe alitimuliwa CCM mwaka 2020 kisha kujiunga na ACT Wazalendo ambapo alipewa nafasi ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo alianza kutofautiana na viongozi wenzake baada ya kusitisha kampeni zake katika uchaguzi huo.

Aidha, tarehe 2 Januari, 2021 Membe alitangaza kung’atuka ACT Wazalendo na huku akieleza huo ni uamuzi wake binafsi na hakulazimishwa na mtu yoyote.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!