Friday , 29 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Membe ‘ampuuza’ Rostam Aziz
Habari za SiasaTangulizi

Membe ‘ampuuza’ Rostam Aziz

Spread the love

BENARD Membe, waziri wa zamani wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, “amemshutumu” mfanyabiashara na mmoja wa wanasiasa mashuhuri nchini, Rostam Aziz, kuwa anajikomba kwa Rais Joh Pombe Magufuli. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, tarehe 17 Mei 2019, Membe alisema, “Rostam asijifanye mtoto mzawa. Mimi na yeye, sote ni watoto wa kambo.”

Membe ametoa kauli hiyo siku moja baada ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, video inayomnukuu Rostam akimataka mwanasiasa huyo kuachana na alichokiita, “harakati zake za kugombea urais katika uchaguzi ujao.”

Membe amekuwa akitajwa na baadhi ya wanasiasa, kuwa anapanga mkakati wa kumng’oa Rais John Pombe Magufuli, katika kinyang’anyiro cha urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza nje ya jengo la Mahakama Kuu, Membe alisema, “Rostam wewe ni mwenzetu, sisi sote tumekatwa mikia. Ukikatwa mkia, hata ukijitahidi namna gani, mkia wako ni mfupi tu.”

Alikuwa akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu video iliyoenea mtandaoni ikimuonesha mfanyabiashara na mwanasiasa huyo maarufu nchini, kuzungumzia mjadala wa urais 2020 na kumshauri Membe asijitose kuwania nafasi hiyo ili Rais Magufuli amalizie awamu ya pili.

Amesema, “…Napata kigugumizi mno kumjibu rafiki yangu Rostam, lakini Rostam ni mchumi na nitakutana naye nimshauri kuwa anafanya vizuri sana katika jamii ya Watanzania anapozungumzia masuala ya uchumi. Lakini azungumze main issues (masuala makuu) ya nchi, siyo personal (watu binafsi), hizi tuwaachie watu wa chini.” 

Amesema, “ni muhimu tukachagua maneno ya kuzungumza kwenye dhamira yetu na mdomoni. Tuzungumze ambacho binadamu watatuheshimu. Kwa level (hadhi) yetu, tunazungumzia masuala ya kitaifa ya uchumi. 

“Kwamba, kwa nini uchumi wetu upo hapa ulipo? Kwa nini wafanyabiashara wadogo na wakubwa wanafunga biashara zao au zile alizozieleza kama economic distortions (upotoshaji wa kiuchumi) tunazijibu.”

Membe ambaye amekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje kwa miaka minane ya utawala wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, anaonekana kuwa tishio kwa Rais Magufuli, ndani na nje ya CCM.

Amesema,”Rostam ni mchumi, hivyo angejikita katika eneo hilo… asijaribu kuwa Mkristo zaidi ya Warumi.”

Aidha, Membe amewataka wanasiasa kuzungumza vitu ambavyo vinaendana na dhamiri zao.

Amesema, ” …tuwe tunazungumza kitu ambacho binadamu anatuheshimu… Nimshauri tu Rostam akubali status (uhalisia), asijaribu kuwa mtoto mzawa wakati mimi na yeye ni watoto wa kambo.” Hakufafanua.

Membe – mwanadipromasia mashuhuri nchini – alikuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania urais kupitia chama hicho mwaka 2015. Alishindwa na Magufuli kwa kile kinachoaminika, kushughulikiwa na kundi lililokuwa linamuunga mkono, Edward Lowassa.

Machoni mwa wengi, mbio za urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, zilikuwa kati ya Membe na waziri mkuu huyo wa zamani. Kambi hizo mbili za Lowassa na Membe, zilikuwa na uhasama mkubwa kuanzia ndani ya jumuiya za CCM.

Lowassa jina lake halikutoka hata ndani ya Kamati Kuu (CC), lakini Membe alifikia hatua ya tano bora, lakini akabwagwa na wafuasi wa Lowassa ambao ndio waliokuwa wengi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu waliokaribu na mwanasiasa huyo, suala la Membe kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao kupitia CCM, “siyo tena jambo la kufikirika.”

“Ninachojua na siyo mimi pekee yangu, karibu sote tunaomuunga mkono, Ndugu Membe, atagombea urais katika uchaguzi ujao. Hapa lije jua au inyeshe mvua,” ameeleza mwanasiasa mmoja ambaye alipata kuwa waziri katika serikali ya Kikwete.

Amesema, “katiba ya CCM haimkatazi mwanachama wake kugombea urais. Kilichopo ni utamadani wa chama, kwamba mwanachama wake ambaye anahudumu kama rais wa nchi kupita bila kupingwa anapoenda kugombea awamu ya pili na ya mwisho ya urais wa nchi. 

“Huo ni utamaduni siyo kanuni, katiba wala sheria. Na Memba hatakuwa wa kwanza. Mwaka 2010, Dk. Mohammed Gharib Billali, alifanya hivyo. Hakuadhibiwa wala hakuitwa msaliti.”

Katika uchaguzi huo, Dk. Billal alijitokeza kumpinga aliyekuwa rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume. Wakati Bilal akijitokeza, Karume alikuwa ametumikia miaka mitano ya kwanza ya uongozi wake.

Taarifa kwamba Membe amekuwa akipanga kuvunja utamaduni huo, zilikolezwa mwishoni mwa mwaka 2018 pale ambapo Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ali, alipomtuhumu mwanasiasa huyo kutaka kuvuruga chama kutokana na mkakati wake wa kutaka kugombea urais.

Dk. Bashiru alisema kumekuwa na taarifa kuwa Membe anajipanga kumkwamisha Magufuli ifikapo 2020.

Alihoji: “Iweje watu waseme kwamba wewe (Membe) unafanya vikao vya kutafuta kura za 2020, kwamba unataka kumkomesha Rais Magufuli, halafu unakaa kimya tu?” 

Kwa sasa, Membe ni mshauri wa masuala ya usalama wa rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, tangu alipochukua madaraka ya urais nchini humo, Desemba 2017 kutoka kwa Robert Mugabe.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

Habari za Siasa

Mgongano wa kimasilahi wamhamisha Chande TTCL

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),...

Habari za SiasaTangulizi

Mgawo wa umeme: Rais Samia ampa miezi sita bosi mpya TANESCO

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amempa miezi sita Mkurugenzi...

Habari za Siasa

Rais Samia avunja bodi ya REA

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua Balozi Jacob Kingu, kuwa...

error: Content is protected !!