July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

‘Mei 3 ni siku ya majonzi’

Spread the love
TAREHE 3 Mei ni siku ya majonzi. Hivi ndivyo linavyoeleza Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anaandika Happiness Lidwino.
Wamesema, ni kwa kuwa Watanzania wanawakumbuka wanahabari waliopoteza maisha yao kwa ajili ya kupigania uhuru wa vyombo vya habari ambao hadi leo bado unaminywa.
Wametamka kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati ikiwa ni siku ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.
Kwa sasa wamesema kuna sintofahamu kubwa kuhusu uhuru wa habari na kwamba, upatikanaji wa taarifa kwa sasa unapita katika wakati mgumu kuliko hata ilivyokuwa wakati wa ukoloni au enzi za tawala za kidikteta.
Roderick Lutembeka, Mwenyekiti wa baraza hilo amesema, vitisho na mashambulizi dhidi ya haki ya kupata taarifa, uhuru wa habari na wanahabari wenyewe ni moja ya viashiria vikubwa vya jamii inayoongozwa na watawala waliojaa hofu.
“Hofu ya kuhojiwa na wasiokuwa tayari kukubali fikra mbadala ndio tatizo kubwa linaloikabili nchi hii kwa sasa.
“Jambo hili ni hatari kwa afya ya taifa. Tunaamini kuwa Watanzania wataitafakari kwa kina na kuifanyia kazi kauli mbiu ya wadau wa habari nchini Tanzania kwa mwaka huu, inayosema “Kupata Taarifa ni Haki ya Msingi, Idai.’
Kuhusu maadhimisho haya, mtandao huu umetaka kupata maoni ya Dk. Azavel Lwaitama, Muhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishirikishi cha Josiah Kibila cha Chuo Kikuu Tumaini-Makumira, Bukoba ambapo amesema, bado kuna sheria kandamizi zinazomimya uhuru wa vyombo vya habari na kumpa mamlaka mtu mmoja kufanya anachojisikia.
“Kwa Watanzania wanaojua mambo machafu yanayofanywa na serikali katika tasnia ya habari, hawawezi kusherehekea siku hii ya leo bali wana majozi kwa yale yanyofanywa kwa shinikizo la mtu mmoja tu anayejiita waziri wa habari ambaye anajifanya kubeba dhamana ya wananchi wote kufungia magezeti na kuamua tu kufuta matangazo ya bunge0” amesema na kuongeza;
“Wananchi kwa muda mwingi walizoea kuona bunge likirushwa kwa pesa za wananchi na tulishazoeshwa hivyo. Pia tulishapiga hatua tukijilinganisha na nchi zingine ambazo zinarusha matangazo ya bunge ‘live’ lakini tumerudi nyuma tena.”
Dk. Lwaitama amesema, kilichofanywa na Bunge ni ukatili wa kuminya habari sahihi kwa wananchi kutokana kwamba, kwa hali ya kawaida taasisi moja haiwezi kukusanya na kusambaza taarifa zilizosahihi.
“Nashangaa serikali hiyo hiyo inapotumbua majipu hadharani, waandishi wanatafutwa lakini wao wanapotaka kutumbuliwa wanafukuza waandishi kwa nini?
“Kunakitu gani hapo kinaendelea? Kwa nini serikali ifanyie mambo yake gizani kama hakuna udikteta na ufisadi?” Amehoji Lwaitama.
error: Content is protected !!