July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Meck Sadick ahimiza usafi kwenye mabasi

Spread the love

MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick amewataka madereva na makondakta kuhakikisha wanaweka masanduku ya taka ndani ya gari na kuzuia abiria kutupa taka kupitia madirisha ya daladala. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Sadick ameyasema hayo leo alipofika katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo (UBT) kwa lengo la kuzindua upuliziaji dawa katika mabasi yaendayo mikoani ikiwa ni moja ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

Wiki kadhaa zilizopita Rais Magufuli aliagiza Siku ya Maadhimisho ya Uhuru kuadhimishwa kwa kufanya usafi nchi nzima ili kutokomeza magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

Akizungumza na wanahabari, Sadick amesema kuwa serikali itahakikisha zoezi la kufanya usafi katika maeneo mbalimbali linakuwa endelevu hivyo watajitahidi kuweka utaratibu wa kufanya zoezi la usafi pamoja na upuliziaji wa dawa katika magari kwa kila wiki.

Ametoa shukrani zake kwa wananchi kwa kupokea amri ya rais Magufuli kwa umoja na kufanya usafi kama siku hiyo ilivyoagiza.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Meneja leseni kutoka Sumatra, Leo Ngowi amesema kuwa siku ya kesho watakaa na na madereva wa daladala na kupanga namna ya kupuliza dawa katika daladala na kuendeleza usafi.

Ngowi amesema kuwa hadi sasa gharama za kupulizia dawa katika daladala hizo bado hazijapangwa na kueleza kuwa huenda bei ikawa ndogo kuliko wanayotoa madereva wa magari ya mkoani.

“Kwa kuwa zoezi hili ni la Tanzania nzima, tunafanya mawasiliano na mikoa mingine ifanye hivi pia ili kuweza kudhibiti magonjwa mbalimbali kuhama kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine,” amesema Ngowi.

Kwa mujibu wa msimamizi wa zoezi hilo la upuliziaji dawa, Mustapha Mwalongo mabasi yaliyopuliziwa dawa yanafikia 70 ambapo inaonekana kuwa ni ndogo kutokana na kutokuwepo kwa mwamko wa wamiliki wa magari kuyapulizia dawa magari yao ambapo kuanzia kesho wanatarajia kupulizia magari mia kwa siku hadi kufikia idadi ya mabasi 1000, idadi iliyopangwa.

error: Content is protected !!