MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Mbeya imemwacha huru, Mdude Nyangali maarufu ‘Mdude Chadema,’ baada ya Jamhuri kushindwa kuthibitisha madai yake kuhusu kusafirisha dawa za kulevya katika kesi ya Jinai Na. 36/2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya…(endelea).
Zawadi Laizer, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, ametoa hukumu hiyo leo tarehe 28 Juni 2021, mkoani humo.
Hakimu Laizer ameeleza kuwepo kwa mashaka ya kuwapo kwa uwezekano kuwa, dawa za kulevya ziliwekwa na polisi nyumbani kwa Mdude ama wakati wa upekuzi au kabla ya upekuzi kufanyika.
Katika maelezo yake, hakimu huyo ameeleza, upekuzi nyumbani kwa Mdude ulikuwa batili kwa kuwa, ulifanywa kinyume cha utaratibu na sheria.
Akieleza hukumu hiyo, Hakimu Laizer amesema, funguo za mshatakiwa huyo, zilikuwa polisi na hazikuchukuliwa kwa namna sheria inavyoelekeza.
Mdude amekaa rumande kwa siku 414 – mwaka mmoja na mwezi mmoja – tangu alipokamatwa Mei 2020 kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin, zenye uzito wa gramu 23.4.
Mdude alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, tarehe 10 Mei 2020, baada ya kufanyiwa upekuzi katika hoteli moja jijini humo, alikokuwa amepanga ambapo alidaiwa kukutwa na dawa hizo.
Hukumu hiyo imetolewa leo baada ya kuahirishwa Jumatatu ya tarehe 14 Juni 2021, kwa kile kilichoelezwa na hakimu sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.
Nje ya viunga vya mahakama, mara baada ya kuachiwa kwa Mdude, shangwe za wafuasi wa Chaadema zilitawala wakati wakitoka mahakamani wakiwa na ‘mtu wao’ Mdude ambaye waliombeba juu juu.
Leave a comment