Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mdude Chadema aibua mjadala, UVCCM yamuonya
Habari za Siasa

Mdude Chadema aibua mjadala, UVCCM yamuonya

Spread the love

 

KAULI ya kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagali ya kutaka kumnyoa kwa wembe Rais Samia Suluhu Hassan, imezua mjadala baada ya baadhi ya watu kumpinga na wengine kumuunga mkono. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Mdude alitoa kauli hiyo  Jumamosi tarehe 1 Julai 2021, mbele ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, katika ufunguzi wa kongamano la kudai katiba mpya, lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Katika kongamano hilo, Mdude alisema wembe alioutumia kumnyoa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, atautumia kumnyoa Rais Samia, kama hatokubali mapendekezo ya upatikanaji katiba mpya.

“Mwambieni huyo mama yenu kuwa, wembe niliotumia kumnyolea mtangulizi wake, nitatumia kumnyolea yeye. Mimi kama kinana nataka kuacga alama katika Taifa hili,” alisema Mdude.

Rais Samia ameingia madarakani tarehe 19 Machi 2021, kufuatia kifo cha mtangulizi wake,  Magufuli, kilichotokea katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam, tarehe 17 Machi mwaka huu.

Kufuatia kauli hiyo, Mwanasiasa na kada wa Chadema, Ally Bananga alionesha kusikitishwa nayo akisema, Mdude alistahili kukaa kimya alipotoka jela badala ya kuanza kuongea majukwaani.

Bananga alisema Mdude alitakiwa akutane na mwanasaikolojia kwanza ili awe imara kimwili, kiakili na kimaono, badala ya kuanza kusimama majukwaani.

“Tulilia wengi alipoteseka gerezani, tulihuzunika sana alipolazimishiwa makosa ya uongo ili apotezwe, tulipigana wengi awe huru, alipotoka jela alistahili kukutana na familia yake. Kuendelea kumpatia kipaza sauti mapema sioni tunachojenga, sioni tukimsaidia, sioni tukimpenda Mdude,” aliandika Bananga katika ukurasa wake wa Instargram.

Mdude alitoa kauli hiyo siku chache baada ya kuachwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, tarehe 28 Juni 2021, kufuatia upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka ya usafirishaji dawa za kulevya, yaliyokuwa yanamkabili mahakamani hapo.

Mdude alisota tumande kwa zaidi ya siku 400, tangu alipokamatwa Mei 2020, kabla Rais Samia hajaingia madarakani.

Licha ya Bananga kuonesha kutofurahishwa na kauli hiyo, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, alihoji kama kitendo hicho cha Mdude kina athari kama alivyosota gerezani bila kuwa na hatia.

“Tuna sema kuwa kauli ya  Mdude katika kongamano la katiba ilikuwa ni kali, ni kweli. Naelewa na pia nafikiri hivyo, lakini je, kali kuliko  kupigwa na kuokotwa porini?  Ni kali kuliko kuwekwa kizuizini. Je , ni kali kuliko kukaa mahabu siku 414 bila kosa?Je, ni kali kuliko  kubambikiwa kesi ya madawa ya kulevya ambayo ingeweza kumfunga jela maisha?” Aliandika Lema katika ukurasa wake wa Twitter.

Lema alishauri Mdude apatiwe msaada wa kisaikolojia badala ya kubezwa” tumsaidie kusahau  bila kumbeza?Wengi hamjui mateso waliyo pitia watu.Mdude atiwe moyo na kuponywa nafsi, ana maumivu makali sana.”

Kutokana na kauli hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kenani Kihongosi, amemuonya Mdude asijitafutie matatizo kwa kutoa lugha chafu dhidi ya viongozi.

“UVCCM inakemea vikali na kuonya tabia za baadhi ya vijana wasiokuwa na maadili wala nidhamu, wanaotumwa ama kujituma kutafuta umaarufu  kupitia jina la Rais  Samia. Hatutovumilia uvunjifu wowote wa heshima kwa rais Wetu. Niwaambie vijana waliokosa nidhamu wajue rais ni kiongozi mkuu wa serikali, mwenye mamlaka kamili. Hivyo wasitafute matatizo yasiyo ya lazima. Heshima ni nidhamu ni vitu vya bure,” amesema Kihongosi na kuongeza:

“Tunamtaka Mbowe atoke hadharani kuomba radhi dhidi ya kauli za Vijana wake, aliokuwa nao katika kikao chake na tunamsihi sana kabla ya kutafuta katiba mpya awafundishe kwanza vijana wake nidhamu, heshima na maadili na ajenge demokrasia ya kweli kwenye kwenye chama chake.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kamati ya Bunge yaitaka Serikali kuchunguza dawa za asili

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo...

Habari za Siasa

Kada NCCR-Mageuzi aliyepotea aokotwa porini akiwa taabani, hajitambua

Spread the love  MWENYEKITI wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha NCCR-Mageuzi,...

Habari za Siasa

ACT Wazalendo yataka Jaji Mkuu, Jaji Biswalo wajiuzulu kupisha uchunguzi fedha za Plea Bargaining

Spread the love  CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimemtaka Jaji wa Mkuu wa Tanzania,...

Habari za Siasa

Kigogo ACT-Wazalendo: Vyama vya upinzani vilikosea kumpokea Membe, Lowassa

Spread the love  KATIBU Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema...

error: Content is protected !!