Tuesday , 23 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mdhamini abanwa ampeleke Lissu mahakamani
Habari za SiasaTangulizi

Mdhamini abanwa ampeleke Lissu mahakamani

Robert Katula
Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imempatia muda zaidi mdhamini wa Tundu Lissu ili amtafute na kumfikisha mahakamani baada ya kushindwa kutokea leo. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, mdhamini huyo, Robert Katula, aliomba muda zaidi wa kuwasiliana na Lissu baada ya kuiarifu mahakama kuwa amesharudi nchini baada ya kuwa nje tangu Septemba 2017 akipata matibabu ya kitaalamu baada ya kushambuliwa kwa zaidi ya risasi 40.

Katula alijikuta akibanwa na hakimu Simba alipoeleza kuwa Lissu hakufika mahakamani kwa sababu “yuko mikoani kutafuta wadhamini kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.”

Hakimu Simba baada ya kumsikiliza mdhamini huyo, na kabla ya kutoa maelekezo, alimuuliza kama binafsi anaridhika kuwa sababu hiyo inakubalika kisheria.

Alipoona mdhamini amekwama kujibu, Hakimu Simba alieleza kwa mkazo kuna umuhimu sababu anayoitoa mdhamini ya kushindwa kufika kwa mtu aliyemdhamini ipimike kisheria vinginevyo hatachoka kumbana.

“Nimekuwa na huruma na wewe na hapa nataka  ujiulize mwenyewe kama hii sababu unayoitoa ina nguvu ya kisheria; maana sisi mahakama ni watekelezaji wa sheria tunaotakiwa kuitazama kila hoja kama inakubalika mbele ya sheria,” alisema Hakimu Simba.

Maelezo hayo yalimsukuma Katula kukumbushia nia yao wadhamini kutaka kujitoa na wamefungua ombi mbele ya mahakama hiyo, maelezo ambayo hakimu hakuyaridhia na akasema:

“Ukileta hayo una maana mahakama ifute dhamana na (wewe mdhamini) uilipie.”

Tundu Lissu-Chadema

Hatua hiyo iliyokuwa mfano wa “mwiba mkali kidondani” kwa mdhamini, ilimlazimu Nyaronyo Kicheere, wakili wa mshitakiwa wa kwanza, Jabir Idrissa, na wa pili, Simon Mkina, kugeuka aliko mdhamini na kumnong’oneza jambo.

Na hapo ndipo Katula alipotamka kuiomba mahakama impe muda zaidi wa kumpata Lissu ili amtake kufika mahakamani siku itakayopangwa kesi kuendelea. Kesi hiyo Na 208/2016, iliahirishwa hadi tarehe 14 Septemba 2020.

“Mheshimiwa naomba muda zaidi wa kumpata mshitakiwa na ninaahidi kumleta mbele yako kesi itakapopangwa,” alisema.

Kauli hiyo ilimtuliza Hakimu Simba ambaye bila ya kusita, alisema, “Sasa haya maneno yanakubalika kisheria… nakupa muda umtafute mshitakiwa na umlete hapa tutakapokutana tena.”

Hakimu Simba awali alisema masuala ya Lissu na harakati za uchaguzi hayaihusu mahakama isipokuwa la muhimu kwa mhimili huo wa kutoa haki ni kutaka afike mahakamani kufuatilia shauri linalomkabili.

Kesi hiyo iko hatua ya usikilizaji lakini ikiwa imekwama baada ya Lissu kushambuliwa kwa risasi tarehe 7 Septemba 2017 na kulazimika kupelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu ya kitaalamu zaidi.

Lissu ambaye ni wakili wa Mahakama Kuu nchini alikimbizwa hospitali ya Nairobi, nchini Kenya baada ya kupata matibabu ya dharura kwenye Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Akiwa hospitali ya jijini Leuven, Ubelgiji, alifanyiwa upasuaji mara 21 katika jitihada za kumsaidia kupona majeraha yaliyotokana na risasi 16 zilizotajwa kumwingia mwilini. Mpaka sasa, hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na shambulio hilo lililompata akiwasili nyumbani kwake eneo la Area D, jijini Dodoma kutoka kuhudhuria mkutano wa bunge.

Katula pamoja na Ibrahim Ahmed waliomdhamini Lissu wakati akiwa bado mbunge wa Singida Mashariki, wamekuwa mara kwa mara wakilazimu kujieleza kutokana na kutofika kwa Lissu mahakamani.

Ombi lao la kutaka mahakama itoe hati ya kukamatwa Lissu linatarajiwa kusikilizwa tarehe 19 Agosti na Hakimu Simba. Kwa muda mrefu   wamekosa mawasiliano naye.

Lissu alirejea nchini tarehe 27 Julai 2020 na kwa sasa anazunguka nchi katika mkakati wa kutafuta wadhamini wa kujaza fomu ya kugombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katula ni Meneja Mkuu wa Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL), kampuni mmiliki na mchapishaji wa gazeti la MwanaHALISI na msambazaji wa MAWIO, gazeti ambalo ndio chimbuko la kesi kutokana na makala iliyochapishwa ikitokana na maelezo ya Lissu kwenye mahojiano yaliyofanywa na Januari 2016.

Mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo ambayo mashahidi wawili walishatoa ushahidi akiwemo aliyekuwa Msaidizi wa Msajili wa Magazeti, Raphael Hokororo, ni Ismail Mehboob, meneja wa kiwanda cha uchapishaji magazeti cha Flint cha jijini Dar es Salaam. 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za Siasa

Rais Samia aridhishwa utendaji mabalozi, awapa neno

Spread the loveRais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza mabalozi  wanaowakilisha ...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

error: Content is protected !!