Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mdee, wenzake wapata kwikwi bungeni
Habari za Siasa

Mdee, wenzake wapata kwikwi bungeni

Halima Mdee
Spread the love

 

BAJETI ya Serikali ya Tanzania kwa mwaka 2021/22 ya Sh.36.3 Trilioni, imepitishwa na Bunge huku wabunge 23 wakishindwa kuikubali au kuikataa ‘abstain.’ Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Kati ya wabunge hao, yumo Halima Mdee na wenzake waliofukuzwa ndani ya kilichokuwa chama chao cha demokrasia na maendeleo (Chadema).

Mdee na wenzake, walifukuzwa na kikao cha kamati kuu ya Chadema kilichokutana Dar es Salaam, tarehe 27 Novemba 2020, kujadili tuhuma za usaliti, kughushi nyaraka za chama kisha kujipeleka bungeni kuapishwa.

Licha ya kufukuzwa Chadema na wao kukiri hadharani kufukuzwa kwao kisha kukata rufaa Baraza Kuu la Chadema kupinga kufukuzwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai amekuwa akisisitiza kuwatambua kama wabunge halali.

Mbali na Mdee, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), wengine waliofukuzwa ni waliokuwa wajumbe wake wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko.

Wengine waliofukuzwa uanachama na Kamati Kuu ya Chadema, ni aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Mwaifunga; aliyekuwa katibu mwenezi, Agnesta Lambat na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.

Katika orodha hiyo, wamo pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

Wengine waliofukuzwa Chadema, ni Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Leo Jumanne, tarehe 22 Juni 2021, Bunge limepiga kura ya kupitisha Bajeti ya Serikali ambapo, wabunge 23 wamepiga kura ya ‘abstain’ (wasiokuwa na upande wowote).

Idadi ya wabunge waliokuwa bungeni ni 385, wabunge watano hawakuwemo bungeni wakati kura zikipigwa, kura 361 sawa na asilimia 94 zimepigwa za ndio na hakukuwa na kura za hapana.

Upigaji kura wa kuidhinisha bajeti ya serikali, umejikita katika Kanuni za Bunge kifungu cha 126 na 92.

Kifungu cha 126(2) kinaeleza; uamuzi wa Bunge wa kupitisha au kutokupitisha Bajeti ya Serikali utafanywa kwa kupiga kura ya wazi kwa kuita jina la mbunge mmoja mmoja.

Ester Matiko, Mbunge asiye na Chama

Pia, kifungu cha 92(10); kinaeleza, baada ya katibu kukamilisha shughuli ya kuhesabu kura, atamjulisha Spika kuhusu kura zote za wanaoafiki, wasioafiki na wasiokuwa na upande wowote na Spika atatangaza matokeo ya hesabu hiyo ya kura.

Hivyo, Mdee na wenzake wamebaki katikakati kuamua kuhusu bajeti hiyo.

Wengine walioungana na Mdee kubaki katikati kwenye kuamua kuipitisha bajeti hiyo ni; Grace Tendega, Asia Mwadin Mohamed, Jesca Kishoa, Nusrat Hanje, Tunza Malapo, Ester Buyala na Esther Matiko.

Pia, wamo Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau, Stella Siyao na Hawa Mwaifunga.

Mbali na Mdee na wenzake, wengine waliopiga kura kama hiyo ni; Shamsia Mkamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini kupitia Chama Cha Wananchi (CUF).

Wengine ni wabunge wa ACT-Wazalendo, Salum Mohamed Shafi (Chonga) na Omar Ali Omar wa Wete.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

error: Content is protected !!