Tuesday , 23 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mdee, wenzake wanaswa mtegoni
Habari za SiasaTangulizi

Mdee, wenzake wanaswa mtegoni

Halima Mdee
Spread the love

 

MIKAKATI mipya ya Halima Mdee na wenzake 18, kutaka kuendelea kuwa bungeni kinyume cha sheria na kukivuruga Chama cha Demokrasia na Maendekeo (Chademo), zimeanza kufichuka. Anaripoti Mwandishi Wetu Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka bungeni Dodoma na kwa watu walio karibu na wanachama hao wa zamani wa Chadema, zinasema wako mbioni kuhakikisha Baraza Kuu la Taifa (BKT) la chama hicho, haliwajadili na kufikia uamuzi wa pamoja wa kuwavua uanachama.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, tayari Mdee “amefikia makubaliano,” na baadhi ya vigogo waandamizi, kuhakikisha wanaendelea kuwa bungeni hadi mwaka 2025 na kuivuruga Chadema.

Aliyekuwa Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), anadaiwa kutaka kupandikiza mgogoro mkubwa ndani ya chama hicho, hususani kwa baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu, pamoja na wa mikoa, ili kukosekane kauli moja ya kufanya uamuzi wa kesi inayowakabili.

“Ni hivi, huu mgogoro sasa umeanza kuwa mkubwa, baada ya baadhi ya watu kutoka upande wa pili, kujitosa kuwasaidia kina Mdee. Lengo hapa ni kutaka Chadema kusiwepo na amani hadi uchaguzi mkuu ujao,” alieleza kada wa chama hicho ambaye mchana yuko chama hicho, usiku kwa kina Mdee.

Mkakati wa Mdee kuivuruga Chadema, unasukwa kwa ustadi mkubwa na baadhi ya vigogo waandamizi ndani na nje ya chama, kupitia rufaa walizowasilisha kwenye Baraza Kuu, kupinga kufutwa uanachama.

Kupatikana kwa taarifa kuwa Mdee na wenzake wanapanga kuzuia Baraza Kuu kuwajadili kumekuja, tangu Chadema wanukuliwe, wakisema wamepokea barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ikiwataka wajieleze kwa nini Kamati Kuu (CC), iliwavua uanachama wanasiasa hao.

Mdee na wenzake, wamewasilisha rufaa Baraza Kuu, kupinga uamuzi wa CC, iliyokutana Dar es Salaam, tarehe 27 Novemba 2021, kuwavua nyadhifa zao za uongozi na kuwafuta uanachama.

Alisema: “Nakwambia hivi, mikakati ni mizito. Mdee huyu, siye yule ambaye mwaka mmoja uliopita, alikuwa anaishambulia CCM na Serikali yake, kwamba inaihujumu Chadema. Huyu ni mwingine kabisa.

“Hawa watu wamejipanga kuzuia kufukuzwa chama, ili kulinda ubunge wao. Nakuhakikishia kama Chadema haitakuwa makini, kikao cha Baraza Kuu, hakitamalizika.”

Katika mkakati huo, pande hizo mbili, zimekubaliana “liwake jua, inyeshe mvua,” Mdee na wenzake, “hawatajadiliwa katika mkutano wa Baraza Kuu na kufikia uamuzi wa kuwafukuza kwenye chama.”

Miongoni mwa mikakati inayopangwa, ni kila mtuhumiwa kuhakikisha anapata wajumbe wasiopungua 10 wa Baraza Kuu watakaowaunga mkono kuzuia kufukuzwa kwao.

“Ni staili ni ileile iliyotumika kwa Lipumba (Profesa Ibrahim), Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),” alisema.

Baraza Kuu la Chadema, linakutana tarehe 31 Julai 2021, jijini Mbeya, linakadiriwa kuwa na wajumbe zaidi ya 350 na ikiwa kila mtuhumiwa atapata idadi ya wajumbe waliyokubaliana, nusu ya wajumbe wa Baraza wataweza kuwa upande wao.

Profesa Lipumba alijiuzulu uenyekiti CUF, katikati ya kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, baadaye mkutano mkuu uliokuwa unaridhia uamuzi wa Baraza Kuu wa kujiuzulu kwake, ulivurugika bila mwafaka.

Siku mbili baadaye, Baraza Kuu lililokutana Zanzibar, likafikia uamuzi wa kumvua uanachama Profesa, lakini ghafla Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, akaibuka na kutangaza kumtambua kuwa Mwenyekiti.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa CC, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa Katibu Mkuu Bawacha, Grace Tendega; aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Baraza hilo (Bara), Hawa Mwaifunga.

Katika orodha hiyo, wamo pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambat; aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mtwara, Tunza Malapo na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha, Zanzibar, Asia Mohamed.

Wengine ni Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Wote walituhumiwa na kutiwa hatiani kwa makosa kadhaa yakiwamo ya usaliti, uchonganishi, kughushi nyaraka, ubinafsi, upendeleo na kujipeleka bungeni kujiapisha kuwa wabunge wa Chadema kinyume cha taratibu na maelekezo ya vikao vya chama.

Mtoa taarifa wetu alisema, mkakati wa kupata wajumbe 10 kwa kila mtuhumiwa, pamoja na mambo mengine, unalenga kumzuia Mwenyekiti, Freeman Mbowe, kuongoza mkutano wa Baraza Kuu.

Alisema: “Hawa wajumbe 10, watatumika kujenga hoja, kwamba kwa kuwa Mbowe ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Kuu; na kwa kuwa kesi iliyofunguliwa na Mdee na wenzake, ni kati yao dhidi ya Kamati Kuu; na kwa kuwa yeye ndiye Mwenyekiti wa kikao kilichofikia uamuzi huo, basi hana uhalali wa kuongoza kikao cha Baraza, kwa kuwa na mgongano wa maslahi.”

Aidha, baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu wanaotafutwa, watamzuia Mbowe kuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, kwa hoja kuwa tayari alishaonesha upande wakati wa ziara zake katika kanda 10 za Chadema, hivi karibuni.
Katika ziara hizo, Mbowe anadaiwa kusema chama chake hakitawasamehe Mdee na wenzake, kwa kuwa “walichokifanya ni kusaliti mapambano ya kutetea haki.”

Kauli za Mbowe dhidi ya Mdee na wenzake, na barua ya malalamiko ya wabunge hao kwa Msajili, kupinga kufutwa uanachama, ni miongoni mwa hoja zinazotajwa kutumiwa na Jaji Mutungi, kuzuia Baraza Kuu kuwajadili wanasiasa hao.

“Hili litafanyika, ikiwa mkakati wa kupata wajumbe wa kuwatetea kwenye Baraza Kuu umeshindikana,” alieleza mtoa taarifa huyo na kuongeza: “Mbali na wajumbe wa kuwatetea ndani, ikishindikana hata vurugu zitafanyika.”

Wakati Mbowe anasema Chadema haitarudi nyuma kwenye sakata la Mdee na wenzake, Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu, naye alisisitiza msimamo wao kama viongozi, hauwezi kubadilika.

Alisema Chadema haina manufaa yoyote na matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita, na ndiyo maana imegoma kutambua matokeo ya uchaguzi huo, kwa kile wanachoita, “mchakato wake haukuwa huru na wa haki.”

Kwa mujibu wa Ibara ya 67 (1) (b), ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, mtu anayepaswa kuwa mbunge, ni lazima awe mwanachama wa chama cha siasa na aliyependekezwa na chama chake.

Nayo Sheria ya Uchaguzi, inavitaka vyama vya siasa, vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, kuwasilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), orodha ya majina ya wanachama wake, wanaopendekezwa kuwa wabunge wa viti maalumu.

Chadema imesisitiza kuwa haijawahi kupendekeza majina ya wabunge wa Viti Maalumu NEC, wala kujaza fomu Namba 8, inayopaswa kujazwa na wanachama wa chama cha siasa, waliopendekezwa na chama chao, kuwa wabunge wanaopatikana kwa njia hiyo.

Chadema imekuwa ikihaha kuhakikisha Mdee na wenzake wanaondolewa bungeni, lakini mara zote uamuzi wao umekuwa ukikumbana na kizingiti kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, anayedai kuwa chama hicho kikuu cha upinzani, hakijawasikiliza waliokuwa wanachama wake hao.

Kama hiyo haitoshi, Spika Ndugai amekitaka chama hicho kuwasilisha kwake, nyaraka zinazothibitisha kufikiwa kwa uamuzi huo, jambo ambalo linapingwa na Chadema kwa maelezo kuwa ni kinyume cha taratibu.

Chadema wanatoa mfano wa wabunge kadhaa, akiwamo Sophia Simba (CCM) na wengine tisa waliokuwa wanachama wa CUF, ambao Spika Ndugai aliridhia kuvuliwa ubunge, bila kuhoji uamuzi wa vikao vilivyofanya uamuzi huo.

Aidha, kwa upande wa CUF, Spika Ndugai aliridhia barua ya Profesa Lipumba ya kuwaondoa bungeni wabunge hao, wakati chama hicho, kikiwa katikati ya mgogoro kati ya viongozi wake wawili wakuu – Lipumba na Maalim Seif Sharif Hamad – na akiwa nje ya nchi.

Hoja ya Chadema, ni kwamba uamuzi wa Spika Ndugai, unapingana na uamuzi wake ya huko nyuma, pamoja na wa watangulizi wake, na kwamba jambo moja na ambalo limeshafika mezani, haliwezi kuamriwa kwa kutumia taratibu mbili tofauti.

“Hii sasa, ni vita. Ni lazima Chadema ijipange, kwa kuwa kati ya wale wabunge, hakuna aliye tayari kurudi nyuma,” alieleza kada mwingine wa chama hicho kwa masharti ya kutotajwa gazetini.

“Hakuna aliye tayari kuomba radhi, kwa kuwa ukiomba msamaha, maana yake, unapoteza ubunge na kila kitu. Ni lazima Chadema watambue, kuwa hii sasa ni vita, na kwamba mustakabali wa baadaye wa Chadema, ni kuishinda vita hii,” alieleza.

1 Comment

  • Nchi kabla ya Chama, na Chama kabla ya Mtu.
    Mosi, imekuwa aibu kwa Bunge lililopokea majina haramu kuiadhibu CHADEMA.
    Pili, wasaliti waondoke na kuanzisha chama chao au wajiunge kwingine.
    Tatu, hizi ndizo siasa za wivu na kinafiki zinazoiaibisha Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za Siasa

Rais Samia aridhishwa utendaji mabalozi, awapa neno

Spread the loveRais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza mabalozi  wanaowakilisha ...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

error: Content is protected !!