August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mdee, wenzake wafungua kesi rasmi kupinga uamuzi wa Chadema

Spread the love

 

HALIMA Mdee na wenzake 18, wamefungua kesi katika Mahakama Kuu Masijala Kuu ya Dar es Salaam kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema, baada ya mahakama kukubaliana na maombi ya kufungua kesi hiyo wiki mbili zilizopita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI Online leo Ijumaa tarehe 22 Julai, 2022 Wakili wao, Edson Kitalu, amesema kesi hiyo namba 36 ya mwaka 2022, imefunguliwa jana ikiwa ni siku ya ukomo iliyotolewa na mahakama kufungua kesi hiyo.

“Hivi sasa Mahakama inaendelea na taratibu zake za kimahakama na pande zote zinasubiri wito kwa kadiri ambavyo mahakama inaona inafaa kuanza kusikiliza kesi hiyo,” amesema Wakili Kitalu.

Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 8 Julai 2022, Mahakama iliwapa siku 14 wabunge hao viti maalum, baada ya kukubali maombi yao , ya kupata kibali cha kufungua kesi dhidi ya Chadema, ili kupinga mchakato wake uliotumika kuwavua uanachama, wakidai haukuwa halali.

Wakili wa Chadema, wakiongozwa na Peter Kibatala (katikati) wakiwa mahakamani

Katika maombi yao, Mdee na wenzake 18, wanaiomba mahakama ifanye mapitio ya kimahakama, dhidi ya mchakato uliotumiwa na Chadema kuwafukuza ndani ya chama hicho, wakidai haukufuata sheria kwa kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa na ulikuwa wa upendeleo.

Mbali na Mdee, wabunge wengine viti maalum wanaopinga kufukuzwa Chadema, ni Jesca Kishoa, Ester Bulaya, Esther Matiko, Hawa Mwaifunga, Grace Tendega, Agnesta Lambart, Cecilia Pareso, Asia Mwadin Mohamed na Felister Njau.

Wengine ni, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Styella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.

Wabunge hao walivuliwa uanachama wa Chadema, tarehe 27 Novemba 2020, ambapo walikata rufaa katika Baraza Kuu la chama hicho, ambazo zilitupiliwa mbali Mei 2022.

Baada ya rufaa hizo kutupwa, Mdee na wenzake 18, walikwenda mahakamani kufungua maombi ya kupinga kuvuliwa uanachama.

error: Content is protected !!