May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mdee, wenzake 18 wamtesa Ndugai

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai analazimika kutoa maelezo ya mara kwa mara kutokana na ‘mashambulizi’ yanayoelekezwa katika kiti chake, kuhusu kushindwa kuwatimua Halima Mdee, wenzake 18 waliokuwa wanachama wa Chadema. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza bungeni leo Ijumaa, tarehe 7 Mei 2021, Spika Ndugai amesema, anashindwa kuchukua hatua katika mgogoro wa wabunge viti maalum 19 waliovuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa kuwa chama hicho hakijakamilisha utaratibu.

Ndugai ametoa kauli hiyo, bungeni jijini Dodoma, akijibu malalamiko ya Chadema kwamba, ofisi yake imeshindwa kuwatimua wabunge hao, ambao wamekosa uhalali wa kuendelea kuwa wabunge.

Spika huyo amesema, Chadema hakijampelekea nyaraka zinazothibitisha maamuzi ya vikao vilivyotumika kuwafukuza wabunge hao.

“Na katika kufanya hivyo lazima wajue nitashirikiana na msajili wa vyama vya siasa, sasa kama sina hivyo viambatanisho, hivi mimi nitajuaje hiyo Kamati Kuu ni kamati kuu ya chama fulani? Anayejua ni msajili.

“Sasa lazima nipate nakala zile, niweze kuona ili niwaite na hao wabunge husika niwaambie ninayo maandishi hapa yanayosema kuna hiki na hiki. Mnasemaje ili nao wajitetee mbele yangu niweze kutoa maamuzi,” amesema Spika Ndugai.

Spika Ndugai ametaja nyaraka anazozihitaji kuwa ni mihutasari ya vikao vilivyotumika kuwafukuza wanachama hao, Katiba ya Chadema.

“Lazima barua hiyo iambatane na Katiba yao, mihutasari ya vikao vilivyohusika katika kuwafukuza wabunge hao, kwa sababu kwa kufanya hivyo inarahisisha kazi yangu ya kutenda haki ili kuweza kuona je, haki imetendeka?

“Kabla na mimi sijaweka baraka zangu nisije kuwoanea watu kwa sababu ambazo hazina mbele wala nyuma,” amesema Spika Ndugai.

         Soma zaidi:

Akizungumzia sakata hilo, Spika Ndugai amesema bila ya utaratibu huo kufuatwa, hatawezi kuchukua hatua dhidi ya wabunge hao.

“Vinginevyo haiwezekani, siwezi toa maamuzi kwa sababu eti fulani anataka jambo fulani halafu ikawa. Haiendi hivyo, ni masuala ya haki na masuala ya haki yanataka utaratibu ulionyooka, hili litatumika kwa mimi na maspika wanaofuata,” amesisitiza Spika Ndugai.

“Anayeandika aambatanishe vitu hivyo, Katiba hii inabadilika badilika, uniletee Katiba inayofanya kazi wakati huu, kwa hiyo wale wenye nia hizo mnaogopa nini kuambatanisha hizo nakala za vikao vyenu? Kwa nini mnaficha ficha? Kuna nini ndani yake? mbona ni jambo rahisi, mnaniletea mimi nafanya kazi yangu.”

Mdee na wenzake 18, walifukuzwa na kikao cha kamati kuu, kilichokutana tarehe 27 Novemba 2020, mkoani Dar es Salaam, wakiwatuhumu kwa usaliti, kughushi nyaraka za chama kisha kujipeleka bungeni kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum.

Mbali na Mdee, ambaye alikuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha), wengine waliofutwa uanachama, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega na aliyekuwa makamu mwenyekiti (Bara), Hawa Subira Mwaifunga.

Katika orodha hiyo, wamo pia Agnesta Lambat, aliyekuwa katibu mwenezi wa Bawacha; Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar; Jesca Kishoa, aliyekuwa naibu katibu kuu wa Bawacha (Bara) na aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje.

Wengine, ni aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo; Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

error: Content is protected !!