July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mdee: Watake wasitake wataachia

Spread the love

HALIMA Mdee, Mbunge wa Kawe amesema, hekaheka zinazofanywa na Serikali, Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi yao ni kutaka kutwaa Umeya wa Jiji la Dar es Salaam lakini wataachia, anaandika Faki Sosi.

“Watake wasitake wataachia, hapa ni Ukawa tu. Yote haya yana mwisho lakini wajue kuwa namba ‘zinatufeva’ na si vinginevyo,” amesema Mdee.

Mdee, Mwita Waitara ambaye ni Mbunge wa Ukonga na washitakiwa wengine watatu leo wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu na kisha kuachwa kwa dhamana.

Washitakiwa hao wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumjeruhi Terresia Mmbando ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano wa kumchagua Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliofanyika Jumamosi wiki iliyopita na baadaye kuhairishwa na kuibua malumbano ya kisiasa.

Washitakiwa wengine kwenye tuhuma hizo ni Shafii Juma, Manase Mjema pamoja na Alfonce Kinyafu, Diwani wa Kimara ambapo kila mmoja amejidhamini mwenyewe kwa Sh. 2,000,000.

Mawakili wa wanasiasa hao ni Peter Kibatala, John Mallya, Omari Msemo, Hekima Mwasibu na Fredrick Kiwelo.

Akizungumza na waandishi wa habari Mdee amesema, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imedai kuwa, hakukuwa na sababu ya kuwakamata isipokuwa ni amri kutoka kwa viongozi wao.

Mdee amesema, jeshi hilo linaendeshwa kinyume cha sheria na kwa matakwa ya wanasiasa na watawala.

“Rais John Magufuli atake asitake ni lazima ataongozwa na Ukawa kwenye Jiji la Dar es Salaam na uchaguzi huu ni lazima Ukawa itashinda kwasababu namba haziwezi kubadilika,” amesema.

Amesema, mahakama imeweka wazi zuio la uchaguzi wa uchaguzi walilopeleka CCM sio halali na kwamba, (CCM) walikua wanatafuta njia ya kuiba kura katika uchaguzi huo.

Waitala ambaye ni Mbunge wa Ukonga amesema hatishwi na kuwekwa rumande na kwamba, wao kuwekwa huko ni sawa na simu iliyoisha chaji na kuchajiwa upya.

“Msimamo umeongezeka, wasimamizi wajipange kwani ukweli upo wazi sasa hakuna figisu,” amesema.

Wafuasi wa Chadema waliofika mahakamani hapo walishangilia kupewa dhamana kwa viongozi wao huku wakiimba ‘Peoples Power.’

Salum Mwalimu, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema amewapongeza watuhumiwa hao na kusema kuwa, hiyo ni moja ya changamoto za ukombozi.

“Tayari tumesikia kuwa wanabuni mbinu mpya ya kuwakamata madiwani ili kuitisha uchaguzi kwa kushtukiza,” amesema.

Mwalimu amesema, chama hicho kimepoteza wanachama wengi kwa kuuawa na wengine wamesingiziwa kesi hatimaye kufungwa.

Kesi hiyo iliyo chini ya Hakimu Mfawidhi Huruma Shahidi, imepangwa kusikilizwa tena tarehe 16 Machi mwaka huu.

error: Content is protected !!