May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mdee, wenzake wamchokonoa Lissu

Spread the love

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tanzania Bara, Tundu Antipas Lissu, amekosoa hatua ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuendelea kuwatambua waliokuwa wanachama 19 wa chama hicho kama wabunge wa Bunge la Tanzania. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Lissu ambaye amepata kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na mbunge wa Singida Mashariki katika Bunge lililopita, ameeleza kuwa ni makossa na uvunjifu wa Katiba, kuendelea kuwatambua watu waliofukuzwa uanachama na chama chao, kuwa wabunge.

“Katiba yetu iko wazi, kwamba mbunge anatokana na chama cha siasa. Spika Ndugai na dunia inatambua kuwa wanaoitwa, wabunge wa Chadema, siyo wanachama wa chama chetu,” ameeleza Lissu katika mahojiano yake na MwanaHALISI Online leo, Jumanne.

Amesema, kuhalalisha kokote kuwa hawa ni wabunge wa Chadema, ni kupindisha sheria na kuvunja Katiba kwa makusudi kunakofanywa na Spika Ndugai. Anahoji: “Hawa wangefukuzwa uanachama na CCM, wangebaki kuwa wabunge?”

Chadema kupitia kikao chake cha Kamati Kuu (CC), kilichofanyika tarehe 27 Novemba mwaka jana, kilitangaza kuwavua unachama wanachama wake 19, wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wake wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Halima James Mdee.

Mdee na wenzake walifukuzwa Chadema, kufuatia kupatikana na hatia ya madai ya makosa ya utovu wa nidhamu, usaliti, kuhujumu chama, upendeleo, kutengeneza migogoro na  kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama.

Mashitaka mengine, ni pamoja na kughushi nyaraka za chama na kwenda bungeni kujiapisha, kinyume na maekelezo na maamuzi ya chama chenyewe.

Wengine waliofukuzwa uanachama, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega; aliyekuwa Makamu Mwenyekiti baraza hilo (Bara), Hawa Subira Mwaifunga; aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; aliyekuwa katibu mwenezi, Agnesta Lambat na naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.

Halima Mdee, Mbunge wa Chadema Viti Maalim

Wapo pia, aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje; aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo; Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba,  Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Kamati Kuu ya Chadema iliyowavua uanachama Mdee na wenzake, ilikutana jijini Dar es Salaam, chini ya mwenyekiti wake wa taifa, Freeman Mbowe.

Licha ya Mdee na wenzake kufukuzwa Chadema, Spika Ndugai ameendelea kuwakingia kifua akisema, mhimili huo utaendelea kuwatambua kama wabunge, na kwamba hatambui uamuzi wa kufukuzwa kwao uanachama.

Akizungumza baada ya kuwaapisha wabunge wawili wa kuteuliwa na Rais John Magufuli (Humphrey Polepole na Riziki Lulida), tarehe 30 Novemba 2020 jijini Dodoma, Spika Ndugai alisema wabunge hao wa viti maalumu ni wabunge halali na wataendelea kuhudhuria mikutano ya Bunge kama kawaida.

Akiandika kupitia ukurasa wake wa Twitter leo, tarehe 2 Februari 2021, muda mfupi kabla ya wabunge hao kuingia bungeni, Lissu alisema, huo ni ufujaji wa fedha za umma kulipa mishahara na posho watu wasiokuwa na sifa ya kuwa wabunge.

“Ni ufisadi na ufujaji wa fedha za umma kwa Bunge kulipa mishahara na posho kwa watu ambao dunia nzima inafahamu hawana sifa ya kuwa wabunge kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.

“Ipo siku wahusika wa ufisadi huu na wale wanaouwezesha watawajibishwa. Tuendelee kukusanya ushahidi,” ameeleza Lissu ambaye alikuwa mgombea urais wa  Chadema, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Kauli ya Lissu inakuja siku tano tokea MwanaHALISI Online liripoti taarifa kuwa Wanawake wa Chadema, kupitia baraza lao – Bawacha – wanapanga mikakati ya kumzika kabisa kisiasa, Mdee na genge lake, kupitia maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Taarifa zinasema, wanawake hao wakishirikiana na baadhi ya viongozi wa majimbo, wameanza kuhamasishana kujitokeza kwa wingi kwenye maadhimisho hayo na kuchangia fedha zitakazoweseha wanawake kufika mjini Iringa, hukudhuria kongamano hilo.

Taarifa zinamnukuu mwenyekiti wa Chadema katika jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam, Patrick Asenga akisema, katika jimbo lake, wameanza kukusanya michango ya fedha zitakazotumika kupeleka wanawake Iringa.

Asenga amesema, “tunatafuta zaidi ya Sh.1.2 milioni, ili ziwasaidie wanawake kwenda Iringa. Hamasa ni kubwa sana. Tunataka kujenga chama na kuonyesha kwenye chama hiki, hakuna aliyebora, kuliko Chadema.”

error: Content is protected !!