WABUNGE viti maalumu, Halima Mdee na Esther Matiko wamemchambua aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli (61), wakisema alikuwa kiongozi wa maendeleo ya vitu hasa miundombinu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Chato … (endelea).
Wanasiasa hao wametoa kauli hiyo jana Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, Chato mkoani Geita, walikokwenda kuhudhulia maziko ya Hayati Magufuli.
Dk. Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya maradhi ya moyo.
Mdee alisema Dk. Magufuli ameacha alama katika sekta ya miundombinu, tangu alipokuwa waziri wa ujenzi hadi Rais wa Tanzania.
Nimekuwa mbunge kwa muda na tulikuwa wabunge pamoja akiwa waziri wa ujenzi. Kitu kikubwa nitakachokumbuka amecha alama kwenye masuala mazima ya miundombinu,” alisema Mdee
“Alikuwa waziri wa ujenzi katika serikali ya Hayati Rais Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete na yeye amekuja kuwa rais, alama kubwa aliyoiacha ni miundombinu kwa mantiki ya barabara, madaraja, vivuko,” alisema Mdee.
Akizungumzia msiba wa Dk. Magufuli, Mdee alisema alishtushwa na kifo chake, kilichotangazwa tarehe 17 Machi 2021 na aliyekuwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ambaye kwa sasa ndiye Rais.
“Nilipokea msiba wa Magufuli nikiwa Dodoma kamati za Bunge zinaendelea, nilipokea kwa mshtuko kama walivyopokea wengine sababu msiba unashtua,” alisema Mdee
Kwa upande wake Matiko alisema, miradi aliyoiacha Dk. Magufuli itasaidia kuondoa changamoto za nchi.
Aliitaja miradi hiyo ni, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), madaraja, barabara, Bwawa kubwa la uzalishaji umeme (Sitigler’s Gorge), mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA).
“Ni mtu ambaye alikuwa anahakikisha Tanzania inaboreshwa katika miundombinu, alijikita sana kwenye maendeleo ya vitu, barabara za kuunganisha mikoa na majimbo.”
“Lami alijitahidi kuweka, alijenga madaraja, SGR, bwawa la umeme ametumia trilioni za hela lakini ukikamilika utatua tatizo la umeme,” alisema Matiko.
Matiko alisema “kupitia mradi wa REA ameleta umeme vijijini. Katika miaka mitano ameweza kuondoa changamoto ya umeme kweye vijiji.”
Mbali na ujenzi wa miundombinu, Matiko alisema Dk. Magufuli ameacha alama ya sera ya elimu bure, ujenzi wa miradi ya maji na hospitali.
Vilevile, Matiko alisema Dk. Magufuli katika uongozi wake alifanikiwa kurudisha nidhamu kwa watumishi wa umma.
Dk. Magufuli alifariki dunia akiwa madarakani, akitumikia muhula wake wa mwisho wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, aliyoutumikia kuanzia tarehe 5 Novemba 2020 hadi 17 Machi 2021, baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Mwanasiasa huyo aliiongoza Tanzania kwa miaka zaidi ya mitano mfululizo, tangu alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza tarehe 5 Novemba 2015.
Mwili wake umezikwa jana Ijumaa nyumbani kwao, Chato mkoani Geita.
Leave a comment