May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mdee awaingiza ‘vitani’ watatu Bawacha

Spread the love

 

WANACHAMA watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamejitosa kusaka nafasi ya kukaimu nafasi ya mwenyekiti wa Baraza la Wanawane la chama hicho (Bawacha) Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ni baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Halima Mdee kufukuzwa uanachama kwa kuasi uamuzi wa juu wa chama hicho.

Wanachama waliochukua fomu kumrithi Mdee ni pamoja na Susan Kiwanga, Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Monica Nsaro na Aisha Luja.

Taarifa hiyo imetolewa jana Jumanne, tarehe 16 Machi 2021, na Makamu Mwenyekiti Bawacha Zanzibar, Sharifa Suleiman ikiwa ni siku moja baada ya zoezi la urudishaji fomu za kugombea nafasi za baraza hilo zilizoachwa wazi, kufungwa.

“Bawacha linapenda kuutarifu umma wa wananchi wote kuwa, zoezi la kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuziba nafasi zilizowazi katika baraza limekamilika tarehe 15 Machi 2021.”

“Wanawake wengi wamejitokeza kuchukua na kurejesha fomu baada ya kujipima na kujiona wanatosha kuziba nafasi zilizotangazwa,” imeeleza taarifa ya Sharifa.

Wanachama 29 wamejitokeza kuwania nafasi sita zilizowazi katika baraza hilo. Nafasi hizo ni, Kaimu Mwenyekiti Taifa, Kaimu Makamu Mwenyekiti Bara, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na Mwenezi.

Nafasi hizo ziliachwa wazi baada ya waliokuwa viongozi wake kufukuzwa kwa madai ya usaliti, kufuatia hatua yao ya kukubali uteuzi wa ubunge viti maalum.

Mbali na Mdee, wengine waliokuwa viongozi wa Bawacha waliofukuzwa Chadema ni aliyekuwa Katibu Mkuu, Grace Tendega; Hawa Mwaifunga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bawacha Bara; Jesca Kishoa, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha na aliyekuwa Katibu Mwenezi Bawacha, Agnesta Lambart.

Kwa mujibu wa taarifa ya Sharifa, wanawake watano wamejitokeza kutaka kurithi nafasi ya Kaimu Mwenyekiti Bawacha Bara, iliyokuwa inashikiliwa na Hawa Mwaifunga.

Wanawake hao ni Elizabeth Mwakimomo, Margreth Kyai, Doroth Namshani, Marietha Chenyenge na Victoria Tindabatangile.

Kwa upande wa nafasi ya Katibu Mkuu Bawacha iliyokuwa inashikiliwa na Grace Tendega, wanawake saba wamejitosa kuiwania.

Wanawake hao ni, Rose Mkonji, Imelda Malley, Ester Daffi, Asia Msangi, Betty Massanja, Rehema Mkoha na Catherine Ruge, aliyekuwa mbunge wa viti maalum na mweka hazina wa baraza hilo

Vilevile, wanawake watano wamejitokeza kugombea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bawacha Bara, akiwemo Brenda Jonas, Mary Muro na Ema Boki.

Wengine ni, Kurwa Nkwera na Amina Kanyama. Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Kishoa.

Bahati Haji, ni mwanamke pekee aliyejitokeza kuwania nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bawacha Zanzibar.

Huku nafasi ya Mwenezi Bawacha iliyokuwa inashikiliwa na Lambart, wakijitokeza wanawake nane kugombea.

Husna Said, Veronica Mwanjala, Paulina Mwaitalako, Zamda Ngonyani na Sarah Bonyo, ni miongoni mwa wanawake waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Wengine ni, Aisha Amme, Aida Mbilinyi na Sirgada Mligo.

Taarifa ya Makamu huyo Mwenyekiti Bawacha Zanzibar imeeleza, baada ya zoezi hilo kukamilika, hatua inayofuata ni vikao maalumu vya kupitia na kuchuja majina.

Sharifa amewataka watia nia wote na wale watakaopitishwa kugombea, kufuata maelekezo ya muongozo na taratibu za kuendesha kampeni za uchaguzi za ndani ya Chadema.

Viongozi hao wa Bawacha na wenzao 13, walifukuzwa Chadema tarehe 27 Novemba 2020, kwa tuhuma za usaliti kufuatia hatua yao ya kukubali uteuzi wa ubunge viti maalumu.

Wengine waliofukuzwa ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu Chadema, Ester Bulaya na Esther Matiko na aliyekuwa Katibu wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Nusrat Hanje.

Wamo pia Tunza Malapo, Cecilia Pareso, Asia Mwadin Mohamed na Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchestea Lwamlaza.

Wanasiasa hao waliapishwa kuwa wabunge na Spika wa Bunge, Job Ndugai tarehe 24 Novemba 2020, kinyume na msimamo wa Chadema kupinga kupeleka wawakilishi wake bungeni kwa madai, matokeo ya uchaguzi mkuu 2020 yaligubikwa na hila.

error: Content is protected !!