December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mdee asema Chadema imewainua wanawake, apata kwikwi kujibu maswali

Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango

Spread the love

HALIMA James Mdee na wenzake 18 wamepata kigugumizi kuweka wazi, mchakato uliofanyika kupatikana kwao hadi kwenda bungeni jijini Dodoma kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Mandeleo (Chadema). Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Mdee na wenzake 18 wamesema, si kweli kwamba ndani ya Chadema kuna mfumo dume kwani, katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, “Chadema ilisimamisha wagombea wengi wanawake kuliko chama kingine cha siasa.”

Hayo yamesemwa na Mdee kwa niaba ya wenzake katika mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika leo Jumanne tarehe 1 Deasemba 2020 jijini Dar es Salaam.

Mdee ameshindwa kujibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua hasa mchakato wa kupatikana kwao ndani ya chama na aliyewapa taarifa wameteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum ni nani.

“Nani alitutuma bungeni, nisema vitu vyote vinavyohusika na kutufikisha hapa, sitazungumza, ndiyo msingi wa kukataa rufaa yetu baraza kuu na sisi kwa sasa tutaendelea kuwa wanachama wa hiali na tukiitwa vikaoni, tutakwenda kama raia wa kawaida,” amesema Mdee.

“Tunakwenda kukata rufaa Baraza Kuu. Tutakwenda kwani kwa sasa hasira zimepungua kila mmoja amecheua hasira,” amesema

“Hatuwezi kujibu ilikuwaje majina yakapelekwa tume na sisi kwenda kuapishwa bungeni kwani tutakuwa tunaelezea mchakato wa ndani, hatuhitaji kupanua mjadala zaidi,” amesema Mdee

Mdee na wenzake 18 walifukuzwa Chadema wakituhumiwa kwa usaliti wa chama hicho kwa kujipeleka kuapishwa tarehe 24 Novemba 2020 na Spika Job Ndugai kuwa wabunge wa viti maalum, wakijua chama hicho, hakijapendekeza majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Uamuzi wa kamati kuu, ulitolewa mbele ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe tarehe 27 Novemba 2020 akisema, Mdee na wenzake wamekisaliti chama na kama hawaridhiki na uamuzi huo, wanaweza kukata rufaa baraza kuu ndani ya siku 30 au kuomba radhi.

Mdee amesema, kuzungumzia ilikuwaje wakafika Dodoma watakuwa wanaingilia mchakato wa ndani wa kukata rufaa “lakini tutakuwa tayari kukubaliana na matokeo ya rufaa.”

Alipoulizwa suala la mfumo dume ndani ya Chadema, Mdee amesema, yeye binafsi pamoja na wenzake, wamefika hapo baada ya kupewa fursa mbalimbali za uongozi, “lakini katika taasisi yotote, changamoto haziepukiki.”

“Siwezi kuzungumzia suala la mfumo dume Chadema kwani Halima Mdee yuko hapa kwa sababu alijengwa kuanzia ngazi ya chini, siwezi kusema kuna mfumo ndume Chadema, katika ujenzi wowote wa taasisi kuna changamoto zake,” amesema

Amesema kati ya hao 19, kwenye uchaguzi mkuu uliopita, 15 walipewa fursa ya kugombea ubunge kwa hiyo, kama kungekuwa na mfumo dume, wasingepewa hiyo fursa.

error: Content is protected !!