May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mdee ‘apindua’ kauli ya Rais Magufuli

Halima Mdee

Spread the love

 

WAKATI Rais wa Tanzania, John Magufuli akisisitiza kwa wananchi ataendelea kutoa elimu bure, Halim Mdee ambaye ni mbunge asiye na chama baada ya kufukuzwa Chadema amesema, ‘si elimu bure ni elimu bila ada.’ Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Kwenye kampeni zake mwaka 2015 na 2020, Rais Magufuli aliahidi na kutimiza azma yake ya elimu bure kuanzia shule za awali mpaka kidato cha nne.

Hata hivyo, Mdee ambaye alitimuliwa uanachama na wenzake 18 kwa kuasi msimamo wa kilichokuwa chama chake (Chadema), amesema badala ya kuita elimu bure, iitwe elimu bila ada.

Amesema, ni kwa kuwa wazazi wanaendelea kugharamia baadhi ya mahitaji ya watoto wao katika elimu hiyo na kilichoondolewa ni ada.

Leo Alhamisi tarehe 11 Februari 2021, Mdee ameitaka serikali iweke wazi kwamba elimu kuanzia shule za awali na msingi hadi sekondari, inatolewa bila ada na sio bure.

Ametoa kauli hiyo baada ya Kipanga Juma Omary, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kusema, serikali inatoa elimu bure kuanzia shule za awali hadi sekondari.

Rais John Magufuli

Mwanasiasa huyo amesema, ametoa wito huo kwa serikali kwasababu kuna baadhi ya shule zinachangisha wazazi michango ya fedha za walinzi na walimu wa ziada.

“Wakati naibu waziri anajibu maswali, amezungumzia neno elimu bure, lakini najua anajua tofauti kati ya elimu bure na elimu bila kulipa ada.”

“Nazungumza hivi kwasababu, kinachofanyika mashuleni huko wanafunzi na wazazi wanatozwa fedha ama za kulipa ulinzi, ama za kulipa maji ama kulipa walimu wa sayansi ambao wanatufutwa wa ziada,” amesema.

Kufuatia madai hayo, Mdee ameitaka serikali kuweka wazi kwamba elimu inayotolewa ni bila ada na sio bure, ili wazazi wajue kwamba wanapaswa kulipa kiasi cha fedha kwa ajili ya michango mbalimbali shuleni.

“Ninachotaka serikali iweke hoja wazi mezani, kinachofanyika ni elimu bila kulipa ada ya Sh. 20,000 na Sh. 70,000 na sio elimu bure, ili wazazi wanapochangia huko wajue kwamba wao katika mchakato wa elimu ya Tanzania, wana sehemu yao ya kuchangia na serikali ina sehemu yao ya kuchangia.

“Kwa hiyo, waweke wazi hapa ni elimu bila ada na sio elimu bure, sababu kwa tafsiri ya kamusi, bure ina maana yake na ada ina maana yake.”

Baada ya swali hilo, Naibu Waziri wa Elimu amesema, waraka wa elimu Na. 5 wa 2015, unaweka wazi kwamba elimu itolewe bila malipo kuanzia shule za awali hadi sekondari.

Hoja hiyo ya Mdee na majibu ya Omary zilionekana kumkanganya Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alitaka ufafanuzi wa kina kuhusu dhana ya elimu bure na elimu bila malipo, kutoka kwa naibu waziri huyo.

Spika Job Ndugai

“Ngoja naibu waziri, kwa hiyo elimu bila malipo sio elimu bure? Nisikuwekee maneno mdomoni, nilitaka uweke vizuri, hebu rudia mwenyewe,” amesema Spika Ndugai.

Akijibu swali la Mdee kuhusu wazazi kuchangishwa fedha, Omary amesema, serikali imeshapiga marufuku michango hiyo.

“Katika muktadha huo, amezungumzia kuna michango wazazi wanachangishwa ya ulinzi, sijui ya usafi, naomba nieleze kuwa serikali katika waraka ule, umebainisha michango ya aina yoyote ambayo mzazi alikuwa anchangia kipindi cha nyuma, sasa hivi hayapo. Gharama zote zinakwenda serikalini,” amejibu Omary.

error: Content is protected !!