September 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mdee amvaa Dk. Mpango bungeni, Spika Ndugai amtetea

Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango

Spread the love

HALIMA Mdee, Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango, amemvaa Dk. Phillip Mpango, Waziri wa wizara hiyo, kufuatia kauli yake ya kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, imeendeshwa kwa mafanikio tangu ilipoingia madarakani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Jana Alhamisi tarehe 11 Juni 2020, wakati akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2020/2021 bungeni jijini Dodoma, alisema Serikali hiyo imeendeshwa kwa mafanikio, tangu ilipoingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015.

Dk. Mpango alisema Serikali ya Rais Magufuli amefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya kiuchumi katika sekta ya ujenzi, uchukuzi na nishati pamoja na ugharamiaji wa huduma za jamii (Afya, Elimu na Maji)

Leo Ijumaa tarehe 12 Juni 2020, Mdee akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kwa mwaka 2020/21, amemtaka Dk. Mpango aeleze mafanikio hayo yako wapi.

“Sio nia yangu kufanya tathimini ya kila lengo, nataka kuonyesha kwamba hiki kitu kinachoitwa mafanikio ya kishindo kama jana kilivyowasilishwa na Waziri Mpango kina walakini mkubwa. Nimalizie kumwambia Dk. Mpango mbwewembwe za jana zilitokana na nini?” amehoji Mdee.

Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe, amesema Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa sugu kwa kutotekeleza bajeti ya miradi ya maendeleo kama inavyopitishwa na bunge.

“Kumekuwa na changamoto ya kutotekelezwa bajeti ya miradi ya maendeleo kikamilifu,  hoja nyingine ya msingi imekuwa kikwazo katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo hapa nchini, ni tabia sugu ya Serikali kutotekeleza kama ilivyopitishwa na bunge,” amesema Mdee

“Hii ni hoja ambayo kambi rasmi ya upinzani bungeni imekuwa ikipigia kelele tangu wakati wa utekelezjai wa mpango wa kwanza wa taifa wa maendeleo, fedha hazipelekwi kama ilivyopangwa.”

Mdee amesema, kushindwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kumethibitishwa jana bungeni na Dk. Mpango, baada ya kusema kwamba Serikali ilishindwa kutoa fedha za utekelezwaji wa miradi hiyo.

Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na MIpango Tanzania

“Hata jana Waziri Mpango ametuthibitishia kwamba katika mwaka wa fedh 2019/2020 mpango wa taifa wa maendeleo ulitenga  Sh. 12.25 Tril. sawa na 37% ya bajeti nzima ya Serikali,  fedha iliyopelekwa mpaka jana ni Sh. 7.63 Tril. tuu,” amesema Mdee.

Wakati huo huo, Mdee amesema Serikali hiyo imeshindwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya kilimo kwa zaidi ya asilimia 80, iliyopangwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka minne iliyokaa madarakani.

“Sekta ya kilimo inakadiriwa kuajiria asilimia 80 ya Watanzania,  bajeti yake ya maendeleo imetekelezwa kwa wastani wa asimilia 17.55 katika miaka yote 4 ya utawala wa serikali hii,” amesema Mdee na kuongeza:

“Ikiwa serikali imetekeleza bajeti ya maendeleo kwa wastani 17.55% inamaana asilimia 82.45 ya bajeti ya maendeleo kwenye sekta ya kilimo haijatekelezwa, kwa maana nyingine asilimia 80 miradi ya bajeti ya mendeleo ya kilimo haikutekelezwa.”

Aidha, Mdee amesema wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wabunge wa vyama vya upinzani wanazungumza lugha moja, katika suala la changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Mdee amesema hata Spika wa Bunge, Job Ndugai, naye mara kadhaa amelalamika juu ya changamoto ya uhaba wa maji katika jimbo lake la Kongwa.

“Unakumbuka hata wewe Spika wakati wa hotuba ya maji ulilalamika sana jinsi jimbo la Kongwa halitendewi haki, tunazunguma lugha moja,” amesema Mdee.

Mara baada ya Mdee kumaliza kuwasilisha maoni ya upinzani, , Spika Job Ndugai amesema mbunge huyo wa Kawe amechokoza moto, na kumuahidi kwamba, atapata majibu yake katika mijadala ya bajeti inayoendelea bungeni hapo.

“Mheshimiwa Halima Mdee ameamua kuchokoza nyuki, amemalizia kwa kuuliza swali la mbwembwe za jana zimetokana na jambo gani?  Naamini mijadala itajibu zilitokana na nini,” amesema Spika Ndugai.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI ONLINE & MwanaHALISI TV kwa habari mbalimbali

error: Content is protected !!