November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mdee aibana Serikali takwimu za Corona, Dk. Mollel ampa makavu

Halima Mdee

Spread the love

 

MBUNGE wa Viti Maalum, Halima Mdee ameitaka Serikali kutoa takwimu sahihi kuhusu Watanzania waliofariki kutokana na maambukizi ya homa ya mapafu COVID- 19 kwa kuwa idadi ya watu 725 iliyotolewa na Serikali haina mantiki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Pia ameitaka Serikali kueleza ni fedha kiasi gani katika mkopo nafuu uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) zimepelekwa kwenye ujenzi wa maabara za upimaji wa maambukizi ya virusi vya Corona. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea)

Mdee amehoji hayo leo tarehe 10 Novemba, 2021 bungeni jijini katika kipindi cha maswali na majibu.

Akijibu maswali hayo ya nyongeza, Naibu waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Dk. Godwin Molel alimtaka Mdee atambue kuwa hiyo sayansi hivyo inahitaji akili kubwa kuyaona na sio hisia za kwenye makorido.

Dk. Mollel ametolea mfano Hospitali ya Bugando kwamba imepatiwa vifaa vya maabara vya kupima Corona vyenye thamani ya Sh bilioni nne, Kibong’oto ambayo ni taasisi ya magonjwa ambukizi zimepelekwa Sh bilioni sita wakati maabara inajengwa kwa thamani ya Sh bilioni 14.

Aidha, katika maswali ya msingi Mdee alihoji ni Watanzania wangapi wamepata maambukizi, wangapi wamekufa na wangapi wamepona tangu janga la Corona lianze.

Pia amehoji ni fedha kiasi gani zimetengwa na  Serikali na zimefanya nini na wapi katika kukabiliana na janga hilo.

Ameongeza nini kinapelekea gharama za kupima COVID-19 kuwa kubwa na ni dawa gani zilizofanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa kwamba zina uwezo wa kuzuia au kutibu COVID-19.

Aidha, amehoji ni tiba gani za asili ambazo ni sahihi kwa Mtanzania ambaye akiugua Covid – 19 anaweza kuzitumia.

Akijibu maswali hayo ya msingi, Dk. Molel amesema hadi kufikia tarehe 25 Oktoba 2021, idadi ya Watanzania 26,164 ndio waliothibitika kuwa na maambukizi. Kati ya hao 725 walifariki na 25,330 walipona.

Amesema takribani kiasi cha Sh bilioni 158 zimetumika kununua vifaa mbambali ikiwemo mitambo 19 ya kuzalisha hewa ya oksijeni yenye uwezo wa kuzalisha mitungi 200 hadi 300 ambapo mitambo 7 tayari imeshasimikwa na 12 ipo katika hatua ya usimikaji.

Dk. Godwin Mollel, Naibu Waziri wa Afya

“Vilevile, Sekta ya afya imepokea kiasi cha shilingi bilioni 466.78 kutoka IMF ambazo zitatumika katika kupambana na UVIKO 19 ikiwemo kujenga na kusimika vifaa katika majengo ya matibabu ya dharura (EMD) 115, ujenzi wa wodi za uangalizi maalum (ICU) 67, ununuzi wa magari 253 ya kubebea wagonjwa, magari 8 ya damu salama,” amesema.

Amesema gharama halisi ya kumpima mgonjwa mmoja ni Dola za Marekani 135 na Serikali sasa inatoza Dola za Marekani 50, hivyo Serikali inachangia Dola 85.

Ameongeza kuwa tafiti mbalimbali zimefanyika duniani kuhusu dawa ila hadi sasa, dawa zilizopo zinatumika kutibu tu madhara yatokanayo na virusi lakini kilichothibitika kwa sasa kusaidia kuondoa vifo ni chanjo.

Kuhusu tiba asili, Dk. Mollel amesema Serikali haijaacha kutumia tiba ya asili kwani Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Mgonjwa – NIMR imepatiwa Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya kuchakata dawa zinazosaidia kutibu Covid- 19.

“Zimetengwa Sh bilioni tatu kwa ajili ya utafiti mkubwa na mgumu ili kuja na chanjo yetu.

“Haya masuala ya kisayansi huwa ni magumu, waachie wanasayansi, inahitaji super computing system kuyaona kwa hiyo tulia!,” alimaliza Dk. Mollel.

error: Content is protected !!