January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mchungaji Mtikila aiokoa CCM

Mch. Christopher Mtikira (kulia) akiteta jambo na Rais Jakaya Kikwete

Spread the love

MWENYEKITI wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amekisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kujinasua na kitanzi cha waamini wa madhehebu ya Kiislamu wanaotaka kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini, ili kuridhia Katiba Pendekezwa. Anaandika Yusuph Jaffar…(endelea).

Vyanzo vya taarifa vinasema, hatua ya Mchungaji Mtikila kushitaki serikali mahakamani, kupinga kuwapo kwa mahakama hiyo, katikati ya upinzani wa Kanisa Katoliki, dhidi ya Katiba Pendekezwa na Mahakama ya Kadhi, kitatumiwa na chama hicho kulaghai Waislamu kuhusu ujio wa mahakama hiyo.

Kesi ya Mtikila imekuja wakati tayari kuna mtafaruku mkubwa serikalini na katika uongozi wa juu wa CCM, kuhusu uwapo wa mahakama hiyo.

Taarifa zinasema, serikali ilikuwa inatafuta namna ya kujiokoa na sokomoko la kukosana na Kanisa ambalo tayari limetangaza na kutaka waumini wake waikatae Katiba Pendekezwa kwa kura.

Taarifa za ndani ya CCM zinasema, hatua ya Mtikila kufungua shauri hilo, kutarahisha serikali kutamka hadharani kuwa haiwezi tena kupeleka muswada wa kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi.

Kwa mujibu wa habari hizo, hatua ya Mtikila kukimbilia mahakamani, itasaidia kuzima dhamira yao iliyojificha ya kuwalaghai Waislam kwa kuahidi kuianzisha mahakama hiyo kisheria.

“Ile dhamira yao haitatekelezeka angalau kwa sasa. Lakini kubwa zaidi ni kwamba wanafurahia mazingira yaliyopo kwa sababu wao hawatalaumiwa tena na Waislam kuwa wameshindwa kutekeleza ahadi aliyoitoa Waziri Mkuu bungeni,” amesema msiri ndani ya CCM.

Ni katika mawazo hayohayo, kunaibuka taarifa kwamba Mtikila ametumwa kusudi kufungua shauri mahakamani kuhusu suala hilo, taarifa ambazo amekataa kuzitolea maelezo fasaha.

Ameiambia MwanaHALISIOnline kwa simu juzi kwamba anachojua yeye lengo lake kwenda mahakamani ni kuzuia mjadala wa Mahakama ya Kadhi kufanywa bungeni kwa kuwa anaamini ni “kinyume cha sheria kwa serikali kujihusisha na masuala yoyote yanayohusu Mahakama ya Kadhi au Shirika la Waislamu Duniani (OIC).”

Waziri Mkuu Pinda, wakati akitoa hotuba ya kufunga Bunge Maalum la Katiba Oktoba mwaka jana, mjini Dodoma, aliahidi umma wa Kiislamu nchini kuwa serikali ikishatafakari kwa upana, itapeleka muswada wa sheria bungeni ya kuanzisha mahakama hiyo kisheria.

 

Ahadi yake ilizua majadiliano muda wote na hadi hivi karibuni Mwanasheria Mkuu mpya wa serikali, George Masaju pamoja na Pinda mwenyewe waliposhikilia kuwa suala hilo halina matatizo na serikali tayari imejiandaa kupeleka muswada kwenye mkutano wa Bunge ulioanza juzi, mjadala ndio umeshika kasi.

Inaonekana wazi kwamba Kanisa limetumia hoja hiyo kuandaa waraka maalum wa kushawishi na kuelekeza wafuasi wake waipinge Katiba Inayopendekezwa, kwa kuipigia kura ya “Hapaha” na kusema hasa kuwa serikali inaridhia kuanzisha sheria ya kuruhusu Mahakama ya Kadhi, jambo linalovunja katiba ya nchi.

Mtikila amekiri kufungua kesi ya kikatiba Na. 14/2015 katika Mahakama Kuu ya Tanzania akitumia hoja hiyo na kwamba anaiomba Mahakama Kuu impe adhabu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kifungo cha muda usiopungua miaka mitano kwa kitendo chake cha kujaribu kuvunja Ibara ya 19 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Ametaka pia Mahakama itamke kwamba ni kinyume cha sheria kwa serikali kujihusisha katika masuala yoyote yanayohusu Mahakama ya Kadhi au Shirika la Waislamu Duniani (OIC).

“Hii ni mihimili mitatu ambayo inapaswa kutoingiliana, nimefanya hivi ili kuzuia kujadiliwa kwa jambo hilo. Haya masuala tumeyaona matokeo yake nchi zingine,” anasema.

Alipoulizwa kuwa, kesi yake inaweza kuisaidia CCM kutokana na kuelemewa na upinzani wa wakuu wa Kanisa, alisema, “sioni sababu ya kuliunganisha suala hili na CCM. Mimi ni kiongozi wa dini na hivyo nasimamia maadili.”

Hata hivyo, aliposhikiliwa kueleza anafikiri si halali kudhaniwa kuwa anatumiwa na CCM kuzima joto la madai ya Waislam kutaka Mahakama ya Kadhi kabla ya kura ya maoni ya kuamua hatima ya Katiba, Mtikila alisema kwa sauti, “Nyinyi sijibu maswali yenu ya kipumbavu.”

“Wewe ni mpumbavu, andika chochote unachotaka,” alisema hata aliponasihiwa kurudi kwenye swali aliloulizwa.

Taarifa za awali zinaonesha kuwa CCM imewekwa kwenye wakati mgumu kutokana na misimamo ya Maaskofu. Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa, inashindwa kurudi nyuma na inaendelea kuwalaghai Waislamu kuhusu mahakama hiyo huku ikitafuta namna ya kutua mzigo huo.

Viongozi wa Kikristo mara kadhaa wamekuwa wakitoa waraka kupinga serikali kutambua Mahakama ya Kadhi; wakiorodhesha hoja zao kama vile kuligawa taifa katika msingi ya udini.

Februari 16 na 17, Baraza la Maakofu Katoliki nchini (TEC), lilikubaliana kupitisha hoja ya kuitaka serikali kusitisha kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na kuwa, maamuzi hayo yalifikiwa na maaskofu wote wa kanisa hilo jijini Arusha.

Waraka huo ulitanguliwa na ule wa Jukwaa la Wakristo Tanzania. Jukwaa hili linaundwa na Taasisi za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT).

Jukwaa hilo lilikutana Machi 10, 2015 na kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na masuala ya usalama wa taifa, Mahakama ya Kadhi na kasha kutoa tamko.

“Mahakama ya Kadhi imekuwa likiendelea kutumiwa na wanasiasa kama mtaji wao wa kujipatia madaraka kwa gharama za kuleta chuki za kidini. Kwa dhamiri safi,

“Jukwaa linatamka wazi kuwa mjadala unaoendelea kati ya Serikali na vikundi vya kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na kisheria ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua juu ya masuala hayo bila kuihusisha serikali wala waumini wa dini nyingine.

“Kwa kuwa Chama Tawala na Serikali wameshindwa kusimamia misingi iliyolea taifa kama serikali isiyo ya kidini na taifa lenye amani; umoja na utulivu;

Jukwaa linawaelekeza waumini wote na wenye mapenzi mema wakati wa uchaguzi mkuu ujao kufanya maamuzi yanayolitanguliza Taifa badala ya kutanguliza mazoea, mapokeo, itikadi na ushabiki wa chama fulani cha siasa.”

Hatua ya Mtikila kufungua kesi kupinda Muswada wa Mahakama ya Kadhi kunarahisishia CCM kupata sehemu ya ‘kuubwaga’ mzigo wa mahakama hiyo na kubaki katika mikono salama kwa upande wa Waislamu na Wakristo.

Katika madai yake, Mtikila amemtuhumu Mwanasheria Mkuu wa  Serikali, George Masaju kushirikiana na Mizengo Pinda, Mary Nagu, Asha-Rose Migiro kwa kile alichokiita kuratibu mchakato wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi.

Mtikila anadai kwamba, kwa mujibu wa sheria za Kiislam (sharia), kiongozi aitwaye “Kadhi Mkuu” anapaswa kuwa na mamlaka ya pili baada ya rais wa nchi. Hivyo, anasisitiza kuwa mfumo huu wa kisheria utawainua waislamu wapatao milioni 12.4 dhidi ya wakristo wapatao milioni 29 hapa nchini Tanzania.

Hata hivyo, Mtikila anamtuhumu pia Stephen Wasira, Mizengo Pinda, Ernest Ndikilo, Karen Yunus, Issa Njiku, Dan Makanga, na Ernest Mangu kwa kile alichokiita kushirikiana na Masaju.

error: Content is protected !!