August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mch. Msigwa aibomoa TCRA, aibeba ITV

Spread the love

MCHUNGAJI Peter Msigwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini ameinanga Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Nchini (TCRA) na kuitaka iache kutumika, anaandika Charles William.

Msigwa ameyasema hayo hii leo kufuatia TCRA kutangaza kukitoza faini ya Tsh. 5 Milioni kituo cha televisheni cha ITV kwa madai ya kurusha kipindi ambacho Msigwa alimkashifu Dk. Tulia Ackson Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Niliwahi kusema Bungeni Kuwa tumezalisha taifa la watu wanafiki, waoga na wanaojipendekeza pendekeza, ITV kosa lao ni nini? Mimi ndiye nilikuwa naongea, aliyenihoji angejuaje kuwa naenda kuongea nilichoongea?” Ameng’aka.

Msigwa amesema kama maneno aliyoyazungumza katika kipindi cha “Kumekucha” kilichorushwa na ITV yalikuwa yanamkashifu Naibu Spika wa Bunge, aliyepaswa kulalamika kukashifiwa ni Dk. Tulia na siyo Mamlaka hiyo ya mawasiliano na pia kama kuna faini aliyepaswa kutozwa ni yeye (Msigwa) na siyo kituo hicho cha televisheni.

“Aliyekashifiwa kwa mujibu wa TCRA ni Ndugu Tulia, yeye ndiye alipaswa kunipeleka mahakamani kama anahisi kukashifiwa. Naiona hii ni njama ya kutisha vyombo vya habari visiwe vinatualika kwenye mahojiano kwenye vipindi vyao,” ameeleza Msigwa.

Msigwa ametadharisha kuwa ni vyema TCRA na mamlaka zingine za serikali zikafanya kazi kwa uhuru na weledi badala ya kufanya kazi kwa hofu na kujipendekeza kwa viongozi wakuu wa serikali kwani hali hiyo inatia dosari utendaji wa mamlaka hizo.

“Watu wamejaa hofu, uoga, mashaka na kutojiamini, maisha ya kujipendekeza ni magumu mno,” amesema Msigwa.

Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania jana ilitangaza kuvitoza faini inayofikia jumla ya Tsh.19 milioni vituo vya utangazaji vya ITV, Clouds TV na Clouds Fm kwa kukiuka kanuni za utangazaji.

AmbapoTCRA ilisema Clouds Media imepigwa faini hiyo kutokana na kosa la kushabikia mapenzi ya mbuzi na binadamu kwenye chombo chao cha habari pamoja na kupiga wimbo wa ‘Ahsanteni kwa kuja’ wa msanii Mwana FA ambao ni wa kudhalilisha utu wa mwanamke na unapaswa kupigwa muda maalum (usiku) kama ambavyo imeagizwa.

ITV wakipigwa faini kutokana na kipindi chake kinachojulikana kama ‘Kumekucha’ ambacho mgeni mualikwa Mchungaji Peter Msigwa Mbunge wa Iringa Mjini anadaiwa kusikika akisema, “Naibu Spika amekuwa kama anavaa pampasi, hataki kubanduka kwenye kiti cha kuongozea Bunge,” maneno yanayodaiwa kuwa ni ya kumkashifu kiongozi huyo wa Bunge.

error: Content is protected !!