September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mchungaji awakumbuka wanafunzi wasiojiweza

Mchungaji wa kanisa la TAG la Swaswa Halisi, Dodoma, Jakson Malendaa

Spread the love

KANISA la Tanzania Asembless of God (TAG) la Swaswa halisi limewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule kwa wale wenye umri wa kwenda shule. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Wito huo umetolewa na Mchungaji wa Kanisa hilo, Msafiri Malenda muda mfupi baada ya kumaliza kukabidhi wanafunzi vifaa vya shule kwa maandalizi ya kufungua shule leo.

Mchungaji Malendaa alisema kuwa kanisa linatambua umuhimu wa elimu ya Dunia pamoja na elimu ya kiimani na kueleza kuwa suala zima la elimu ni mpango wa kimungu.

Mchungaji huyo alisema kuwa kanisa limekuwa na utamaduni wa kutoa vifaa vya shule kwa wanafunzi ambao wanaishi katika mazingira magumu na wanaoishi katika familia duni ili watoto hao nao waweze kupata elimu kama ilivyo kwa watoto wengine.

Mbali na kanisa hilo kutoa misaada kwa wanafunzi wanaotoka katika familia masikini na wanaoishi katika mazingira magumu Mchungaji Malendaa alisema kuwa misaada hiyo haibagui mwanafunzi kutokana na itikadi za kidini wala kisiasa na kueleza kuwa suala la elimu ni kwa watu wote.

“Kanisa limetoa vifaa vya shule kwa wanafunzi wote ambao wanatokea katika familia masikini na wale wanaoishi katika mazingira magumu bila kujali itikadi za dini zao, lakini wakati wa ugawaji walijitokeza watoto wengine ambao wanaishi maisha ya kawaida na kwa kuwa walikuwa katika eneo la tukio nao waliweza kupatiwa vifaa vya shule.

“Kanisa linatoa msaada huo kwa kutimiza maandiko kwani neno la Mungu linasma “ishikeni sana Elimu isije ikaenda zake” kwa maana hiyo elimu ni jambo muhimu sana kwa kuwapatoa watoto na hata watu wazima , na kwa maana hiyo tunawahimiza wazazi au walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule kwa wale wenye umri wa kwenda shule kwa maana ya shule ya msingi na sekondari,” alisema Mchungaji Malendaa.

Katika hatua nyingine mchungaji huyo alisema kuwa katika kujenga usawa na kuwafanya watu wote kuonekana kuwa ni swa kanisa hilo limeweza kutoa msaada wa chakula kwa familia ambazo hazina uwezo ili nao waweze kupata chakula na kujiona kuwa ni sawa na jamii nyingine.

Kutokana na hali hiyo mchungaji Malendaa ameiomba jamii kuona uwezekano wa kuwasaidia watoto ambao wanashindwa kwenda shule kwa kukosa vifaa mbalimbali vya shule na kueleza kuwa iwapo watawasaidia watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu watakuwa wametoa sadaka njema kwa Mungu.

error: Content is protected !!