SHEKANDI Ashery Mkombola (44), Mchungaji wa Kanisa la Aglikana, lililopo katika Kijiji cha Chinyika, Mpwapwa jijini Dodoma, na watu wengine 21 wanatuhumiwa kukutwa na vipande18 vya meno ya Tembo. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Gilles Muroto, watuhumiwa hao walikamatwa katika matukio mawili tofauti, ambapo mchungaji Mkombola amedaiwa kukutwa akisafirisha meno mawili ya Tembo yenye uzito wa kilogram 15.
“Mchungaji huyu alikamatwa katika Kijiji cha Pwaga, kilichopo tarafa ya Kibakwe ingawa anaishi Kijiji cha Mungui na alikua akisafirisha meno hayo kwa kutumia pikipiki aina ya Fekon, yenye namba za usajili MC 772 AYK,” amefafanua Kamanda Muroto.
Amesema, katika tukio la pili watuhumiwa wawili ambao majina yao yanahifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi, wamekamatwa katika stendi ya mabasi ya nane nane jijini Dodoma wakiwa na vipande 16 vya meno ya Tembo, wakiwa wamevificha katika dumu la lita 20 lililokatwa juu.
Katika tukio jingine, Kamanda Muroto amesema polisi inawashikilia watu wawili – Sam Ally Isihaka (44), dereva wa gari aina ya Benz lenye namba za usajili AIB 5596 na Mwinyi Ramadhani Magumila (47), dereva wa gari aina ya Benz lenye namba za usajili AIB 6924 kwa kosa la kukwepa ushuru.
Amesema, watuhumiwa hao wakiwa safarini kuelekea Rwanda, walikwepa ushuru wa serikali katika mizani ya Uyole Mbeya, Makambako, Njombe na Wenda Tanangozi Iringa kwa kushawishi na kutoa rushwa kwa maofisa wa mizani.
“Maafisa hawa wa mizani nao walipokea rushwa na kutoa risiti bandia, ili kuruhusu magari hayo mali ya kampuni ya Reginal Logistics ya Dar es Salaam kupita bila kupima. Walikuwa wamezidisha uzito wa mizigo zaidi ya 650 grm yaani gross vehicle mass,” amebainisha Kamanda Muroto.
Kufuatia tukio hilo, Muroto amesema watuhumiwa sita wakiwemo maofisa wa mizani waliokuwa zamu katika vituo hivyo, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na wanatarajia kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Leave a comment