RAIS wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), anayemaliza muda wake, Dk. Lugemeleza Nshala amesema, uchaguzi wa viongozi wa chama hicho 2021, umezungukwa na mchuano mkali, ikilinganishwa na chaguzi zilizopita. Anaripoti Regina Mkonde, Arusha … (endelea).
Dk. Nshala ametoa kauli hiyo leo Jumatano tarehe 14 Aprili 2021, wakati anazungumza na MwanaHALISI Online jijini Arusha.
TLS kinatarajia kufanya uchaguzi wa rais, makamu wa rais na mweka hazina, Ijumaa tarehe 16 Aprili 2021.
Akizungunzia uchaguzi huo, Dk. Nshala amesema, mchuano huo ni mkali kwa kuwa wagombea wake wana ushawishi mkubwa, sambamba na uchaguzi huo kufuatiliwa na watu wengi nchini.
“Sasa kuna mchuano mkali, inaonesha TLS ina umihumu sana katika kuhakikisha nchi inaongozwa kwa misingi ya sheria,” amesema Dk. Nshala.
Wanaochuana kurithi mikoba ya Dk. Nshala ni, Dk. Edward Hoseah, Flaviana Charles, Shehzada Walli, Francis Stolla na Albert Msando.
Kauli hiyo ya Dk. Nshala imekuja katika kipindi cha lala salama, ambapo kampeni zake zinatarajiwa kufungwa kesho Alhamisi tarehe 15 Aprili 2021.
Mbali na uchaguzi wa viongozi wa ngazi za juu, TLS leo kimefanya uchaguzi wa viongozi wa kanda na wa chama cha wanasheria vijana.
Viongozi watakaoshinda katika chaguzi hizo, wataapishwa Jumamosi tarehe 17 Aprili 2021.
Leave a comment