OFISA wa Jeshi la Polisi katika Jimbo la Hai, Mkoani Kilimanjaro, anachunguzwa na jeshi hilo kwa madai ya kumtabiria Freeman Mbowe, mgombea ubunge wa jimbo hilo kung’olewa kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro…(endelea).
Taarifa ya kuchunguzwa kwa ofisa huyo, imetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro.
IGP Sirro amesema, timu ya kuchunguza video ikimuonesha ofisa wa jeshi hilo akitamka kwamba, Mbowe hatoshinda jimboni humo, kutoka Makao Makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam, tayari imetua mkoani humo kwa ajili ya kuanza kazi.
Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho Taifa, ni mgombea wa jimbo hilo anayetetea kiti chake ambapo video hiyo ilimuonesha akiwa anazozana na ofisa huyo.

Wakati wakizozana,ofisa huyo alimwambia Mbowe “utamshinda yule? huwezi kumshinda, unawadanganya wananchi kuwa utamshinda.”
Video yenye kauli hiyo, ilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha ofisa huyo aliyekuwa amevalia sare za polisi, akionesha kukerwa na wananchi kumfuata Mbowe huku akimtaka aingine kwenye gari.
Hata hivyo, Mbowe alimtaka ofisa huyo kutowatimua wafuasi wake waliokuwa wakimfuata.
Awali ofisa huyo alisema “mnafanya watu wanakuja. Ingia kwenye gari tuondoke,” Mbowe alijibu “sawa, msifukuzie watu wangu, watu wanifuate niwakimbie, hapana!”

Na kisha ofisa huyo akamwambia Mbowe “huwezi kumshinda hata ufanyeje, humshindi, ingia kwenye
gari uondoke, yaani mawazo yako unawadanganya wananchi utamshinda, humshindi.”
IGP Sirro amekiri kuona video hiyo ambapo amesema, timu ya uchunguzi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la
Polisi, imekwenda kulichunguza tukio ili kuwa na majibu yanayojitosheleza.
Leave a comment