January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mchango wa wanawake katika historia kutambuliwa

Bibi Titi Mohamed mmoja kati ya wanawake walioingia kwenye historia ya Tanzania

Spread the love

KAMPENI ya kutambua na kuenzi mchango wa wanawake katika historia ya Tanzania itazinduliwa 27 Machi mwaka huu. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Lengo kuu la kampeni hiyo ni kuwaenzi wanawake wote waliofanya vizuri katika kuleta maendeleo katika ngazi ya jamii hadi kitaifa.

Wanawake watakaoenziwa ni wale wanaojulikana na wasiojulikana na hawatajwi mahali popote katika historia ya nchi japo wana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo na kutengeneza historia ya nchi.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Lilian Liundi- Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)- amesema kampeni hiyo itaongozwa na dhima inayosema “Uthubutu wa mwanamke na miaka 54 ya maendeleo ya Tanzania”.

“Malengo mahususi ya kampeni ni kutafiti na kukusanya taarifa muhimu za michango ya wanawake katika maendeleo na historia ya nchi kijamii, kiuchumi na kisiasa,” amesema Liundi.

Malengo mengine ni kuhamasisha wananchi kushiriki katika kuibua na kutoa taarifa zilizopo na zitakazo kusanywa na kuzihifadhi katika makumbusho na sehemu nyinginezo kwa njia ya digitali na makala;

Kutumia taarifa hizo kuwaenzi wanawake kama sehemu ya kuhamasisha vizazi vya sasa na vijanvyo umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika maendeleo endelevu. Kuendeleza mijadala kuhusu michango na ushiriki wa wanawake na kudai uelekezaji wa rasilimali kutoka kwa wadau mbalimbali katika kuendeleza ushiriki wanawake na kuwaenzi.

“Kampeni itakuwa na awamu tatu. Kilele cha awamu ya kwanza kitakuwa ni wakati wa tamasha la jinsia ambapo chapisho maalumu, makala ya video, onyesho maalumu vitaandaliwa. zawadi mbalimbali kwa wanawake watakaokidhi vigezo vinavyoonesha mchango mkubwa katika maendeleo na historia ya nchi zitatolewa,” ameongeza Liundi.

Kampeni hiyo itachukua miaka mitatu. Inatarajiwa kuhusisha wadau mbalimbali wakiwemo TGNP Mtandao, Makumbusho ya Taifa, Women Research Development Project, Women Fund Tanzania (WFT), Soma na Shule ya Uandishi wa Habari ya RAIDA.

Pia mashirika ambayo yanahusika katika kutetea haki za wanawake na usawa wa kijinsia nayo pia yatahusishwa katika kampeni hii.

error: Content is protected !!