RAIS John Magufuli anatarajia kupokea ripoti ya pili kuhusu usafirishaji wa mchanga wa dhahabau (maknikia) Jumatatu ya tarehe 12 Juni mwaka huu, ikiwa ni wiki tatu tu tangu apokee ripoti ya kwanza iliyosababisha kung’olewa madarakani kwa Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, anaandika Hamis Mguta.
Kamati ya kwanza iliyongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma illiundwa wataalamu wa masuala ya jiolojia, kemikali na uchambuzi wa kisayansi, lakini kamati ya pili iliyo chini ya Prof. Nehemiah Eliachim Osoro na ambayo itawasilisha ripoti yake Jumatatu imesheheni wachumi na wanasheria tu.
Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, amesema tukio hilo litarushwa hewani moja kwa moja kupitia redio, televisheni, mitandao ya kijamii na tovuti rasmi ya Ikulu ambayo ni www.ikulu.go.tz kuanzia saa 3:30 asubuhi.
Rais Magufuli alipokea ripoti ya kamati ya kwanza yenye wajumbe wanane Mei 24, mwaka huu iliyochunguza viwango vya madini yaliyomo kwenye mchanga wa madini uliomo ndani ya makontena yaliyozuiliwa na Serikali kusafirishwa nje ya nchi.
Kamati hiyo iliteuliwa na Rais Machi 29, mwaka huu. Huku Kamati ya wanasheria na wachumi ikiteuliwa Aprili 10 mwaka huu.
Baada ya kuipokea ripoti hiyo, Rais Magufuli aliytengua uteuzi wa Prof. Muhongo huku akiahidi kuchukua hatua zaidi baada ya kupokea ripoti ya pili.
Sambamba na uamuzi huo lakini pia Rais aliivunja Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na kumsimamisha kazi mkurugenzi mtendaji wake.
Leave a comment