January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mchakato wa wabunge viti maalum waiva

Spread the love

TUME ya taifa ya uchaguzi imesema kuwa ndani ya siku tatu kuanzia leo itaweka hadharani majina ya wabunge wa viti maalum na kila chama kitafahamu idadi ya wabunge kiliopata. Anaandika Charles William … (endelea..)

Wabunge wa viti maalum ambao hupendekezwa na vyama vya siasa vilivyofanikiwa kufikisha asilimia tano ya kura zote za wagombea ubunge wa chama husika wanatarajiwa kuwa asilimia 40 ya wabunge wa majimbo yote 264 ikiwa ni mjumuiko wa majimbo ya Tanzania Bara na Visiwani.

Akizungumza kwa njia ya simu na MwanaHALISI Online Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima amebainisha kuwa mchakato wa kukokotoa asilimia za kila chama na idadi ya wabunge ambao kila chama kitapata umekamilika na kilichobaki sasa hivi ni maandalizi ya mwisho ya kuyatangaza majina hayo.

“Isingekuwa leo ni mapumziko ya kitaifa na kazi zimesitishwa tungeweza kuyaweka hadharani majina ya wabunge wa viti maalum mapema zaidi lakini kwa sababu hiyo tutayatangaza ndani ya siku tatu kuanzia leo Alhamisi,” ameeleza Kailima.

Kailima amewaomba wanahabari na vyama vya siasa kuvuta subira ili majina hayo yaweze kutangazwa na Tume kwa mujibu wa sheria na kukata kiu ya kusubiri nafasi hizo ambazo husaidia vyama vya siasa kuongeza idadi ya wabunge na hivyo kuwa na nguvu zaidi ya kufanya maamuzi ndani ya bunge.

Hapo awali ilitarajiwa kuwa tume ya taifa ya uchaguzi ingewahi zaidi kuyatangaza majina ya viti maalum ili wabunge ambao wangependa kuhudhuria uapishwaji wa Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano siku ya leo wapate fursa ya kufanya hivyo.

Miongoni mwa vyama 21 vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka, huu ni vyama vitatu pekee vinavyotarajia kupata mgao wa wabunge wa viti maalum kutokana na wagombea wake kufanya vizuri katika nafasi za ubunge, vyama hivyo ni Chama Cha Mapinduzi(CCM), Chadema na Chama cha wananchi-CUF.

error: Content is protected !!