CHAMA tawala nchini Tanzania- Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema wakati wowote kuanzia sasa, kitaitisha mkutano mkuu maalum wa kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa Mwenyekiti wa chama hicho. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Ni baada ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Rais John Pombe Magufuli (61), kufariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Baada ya kifo hicho, Mama Samia, aliyekuwa makamu wa Rais wa Tanzania, amekwisha kuapishwa kuwa Rais, kumalizia kipindi cha miaka minne na ushehe kati ya mitano ya serikali ya awamu ya tano.
Leo Jumamosi, tarehe 20 Machi 2021, kikao cha kamati kuu ya CCM kilikutana baada ya kuitishwa na makamu wenyeviti wa CCM, Philip Mangila wa Bara na Dk. Ali Mohamed Shein wa Zanzibar.
Kikao hicho, kimefanyikia ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, jijini Dar es Salaam ambapo, Humphrey Polepole akizungumza na waandishi wa habari kutoa kilichojadiliwa amesema, chama hicho, kina imani na Mama Samia ‘’mama shupavu’’ kwamba atatekeleza kwa makini miradi yote, iliyoanzishwa na kuahidiwa na Dk. Magufuli wakati wa kampeni.
Kuhusu mkutano huo, Polepole amesema ‘’ndani ya muda mfupi kutoka leo, utaitishwa mkutano mkuu maalum ukiwa na agenda moja ya kupendekeza jina la mwenyekiti wa chama na jina hilo ni la Mama Samia Suluhu Hassan.’’

Amesema, mkutano huo mkuu ‘’lazima uandaliwe. Mkutano huu hutanguliwa na mikutano mingine kama wa kamati kuu na mkutano wa halmashauri kuu ya CCM.’’
Polepole ametumia fursa hiyo, kuwataka wanachama wa chama hicho wa Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar na Chato kujitokeza kwa wingi, kuuaga mwili wa Dk. Magufuli, aliyejitoa kulitumikia taifa hilo.
Leave a comment