Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mchakato kumtafuta mrithi Maalim Seif kuanza Alhamisi
Habari za SiasaTangulizi

Mchakato kumtafuta mrithi Maalim Seif kuanza Alhamisi

Spread the love

 

CHAMA cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, kitaanza mchakato wa kumpata mrithi wa Maalim Seif Sharif Hamad (77), kwenye nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar, Alhamisi tarehe 25 Februari 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mchakato huo, utaanza baada ya Maalim Seif, ambaye pia, alikuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, kufariki dunia asubuhi ya tarehe 17 Februari 2021, katika hospitali ya taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, alipokuwa amelazwa tangu 9 Februari.

Mwamba huyo wa siasa za Zanzibar, alifikwa na mauti baada ya kuwa amekaa kwenye wadhifa huo wa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa siku 71, tangu alipoapishwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi.

Maalim Seif Sharrif Hamad, Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, jina la mpendekezwa wa kumrithi Maalim Seif linapaswa kumfikisha Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010, haijazungumzia muda ambao chama kilichotoa makamu wa kwanza au wa pili wa Rais, akifariki dunia, kiteue mwingine.

Hata hivyo, Ibara ya 40 (2) inasema; Iwapo mtu atafutwa katika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mujibu wa kijifungu cha (1)(b) cha kifungu hiki, chama chake si zaidi ya siku 14, kitapendekeza kwa Rais jina la mtu mwengine.

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu akizungumza na MwanaHALISI Online leo Jumatatu tarehe 22 Februari 2021, amesema, bado wanaendelea na maombolezo ya siku saba ya Maalim Seif, yanayomalizika Jumatano ya 24 Februari.

“Sisi tupo bado kwenye msiba wa kuondokewa na mwenyekiti wetu, kipenzi chetu, Maalim Seif na kwa sababu bado tupo kwenye maombolezo kwa siku saba. Tutaendelea kuomboleza hadi muda huo uishe na mchakato wa nani wa kurithi Maalim Seif utatolewa,” amesema Ado

Wakati Ado, akisita kuweka wazi, lini kikao hicho kitafanyika, MwanaHALISI Online, limezungumza na baadhi ya viongozi waandamnizi wa chama hicho, ambao wamesema, kikao hicho kitafanyika kati ya Alhamisi au Ijumaa wiki hii.

Hata hivyo, viongozi hao wameshindwa kuweka wazi, nani anayepewa nafasi, lakini wanachama watatu wa chama hicho, wanapewa fursa kubwa ya kumrithi Maalim Seif.

Wanaopewa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, ni Masour Yusuf Himid, Othman Masoud Othman na Juma Duni Haji, maarufu kama ‘Babu Duni.’

Babu Duni ni Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Zanzibar), ambaye ameshiriki harakati za kupigania demokrasia visiwani, karibu robo ya umri wake wa miaka 71 sasa.

Juma Duni Haji

Mwaka 2015, akiwa Chama Cha Wananchi (CUF), Babu Duni, ambaye ni mzaliwa wa Unguja, alihamia Chadema na kuwa mgombea mwenza wa urais wa Edward Lowassa.

Baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo na Lowassa, ambaye ni waziri mkuu mstaafu, Babu Duni, alirejea tena CUF.

Babu Duni na Maalim Seif, pamoja na viongozi wengine kadhaa, walikihana chama hicho na kujiunga na ACT-Wazalendo, mwaka 2019, kufuatia kuibuka kwa mgogoro wa muda mrefu ndani ya chama hicho ambacho walikiasisi.

Babu Duni ametajwa kuwa mmoja wa wafuasi wa karibu wa Maalim Seif na aliwahi kutajwa kumpinga kiongozi huyo katika nafasi ya urais katika miaka 2000, lakini Babu Duni mwenyewe akajiweka mbali na mradi huo.

Babu Duni aliyewahi kuwa katibu mkuu wa wizara kadhaa na waziri wa afya kati ya mwak 2010 hadi 2015, anapewa fursa ya kumrithi Maalim Seif, kwenye nyadhifa zote mbili za Makamu wa Kwanza wa rais na mwenyekiti wa chama hicho.

Mwingine anayepewa nafasi ya kuvaa viatu vya Maalim Seif, ni Othuman Masoud, ambaye alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali ya Zanzibar.

Othuman Masoud

Mara baada ya Dk. Shein, kuingia madarakani mwaka 2010, alimteua Othuman kuwa mwanasheria mkuu wa serikali Novemba 2010; nafasi aliyohudumu hadi Oktoba mwaka 2014, uteuzi wako ulipotenguliwa.

Othuman alikumbana na dhahama hiyo, kutokana na misimamo yake, kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Zanzibar, kwenye mchakato wa kutafuta Katiba Mpya.

Othuman, alikuwa muumini wa serikali tatu na kupigania kupunguza mambo ya muungano na kupiga kura ya wazi ya kupinga mambo kadhaa yahusiyo Zanzibar, jambo lilikuwa tofauti na msimamo wa CCM.

Kutokana na msimamo huo, Othuman alitimliwa ndani ya Bunge Maalum la Katiba, jijini Dodoma na kurejeshwa Zanzibar, ambako nako, alikutana na rungu la Dk. Shein la kumvua wadhifa huo.

Othuman ambaye ni mzaliwa wa Pandani, Pemba, mbali na shughuli zake za kisheria anazozifanya ndani na nje ya Zanzibar, ameendelea kusimamia msimamo wake wa haki ya Wazanzibar akiamini kwenye serikali tatu, kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif.

Ni miongoni mwa wanachama wenye kupanga mikakati ya ndani ya ACT-Wazalendo ya kuweza kuibuka mshindi na kwa kipindi chote, amekuwa karibu na viongozi wakuu wa chama hicho.

Othuman alianza kuwa karibu na Maalim Seif, katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020, na alikuwa miongoni mwa timu maalum iliyoandaa ilani ya uchaguzi huo kupitia ACT-Wazalendo.

Katika kundi la wanaotajwa kumrithi Maalim Seif, yupo pia Mansour Yusuf Himid, ambaye amepata kusika nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwamo waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, wakati wa utawala wa Amani Karume.

Mansour Yusuf Himid

Alishika pia wadhifa wa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM na Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho Zanzibar na Katibu wa Fedha na Uchumi Visiwani.

Mansour alikuwa mjumbe wa Kamati ya Mwafakala iliyoongozwa na mwanasiasa mkongwe Visiwani, Hassani Nassoro Moyo.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV kwa habari za kina kuhusu kinachoendelea kwenye mchakato huu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

error: Content is protected !!