June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbwembwe si kipimo cha uongozi- wasomi

Waziri wa Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu aliyejiuzuru, Edward Lowassa

Spread the love

WACHAMBUZI wa masuala ya kisiasa, wamekosoa mbwembwe zinazofanywa na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotangaza nia ya kuomba uteuzi wa kugombea urais kupitia chama hicho, wakisema sio kipimo cha ama wanafaa au la. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Mhadiri Mwandamizi wa Chuo cha Tumaini, Dk. Azavel Lwaitama, anasema pamoja na hekaheka kubwa za wagombea lakini zipo njia za kuthibitisha kufaa au kutofaa kwake.

“Kwanza tujue anatoka chama gani? Chama hicho kina sifa gani lakini pia je aliwahi kutetea maslahi ya umma alipokuwa kwenye uongozi? Na wala si kupelekwa na upepo wa hekaheka zao,” anasema.

Dk. Lwaitama anasema, kipindi hiki kila mgombea anataka kuwaonesha wananchi kwamba anafaa lakini pia kwa wananchi wanapaswa kuonesha kuwa wamekomaa.

“Wagombea hawa pamoja na kujitokeza kwa mbembwe lakini tuwapime. Je, ni wasafi kwa kiasi gani? kwanini wanatumia nguvu kujitangaza? Malamiko ya wananchi katika chama hicho aliyateteaje? amehoji.

Anasema, wapo wanaojitokeza kutaka kugombea lakini hao hao chama wanachotaka kugombea tayari kimewaita fisadi na chama hakijawasafisha na kimetembea nchi nzima kutaka avue gamba, “na wakimpitisha mtu wa namna hii mimi nitawashangaa sana.”

Dk. Lwaitama anasema, wananchi wanapaswa kukumbuka ni kwa namna gani wanaojitokeza walipambana na hoja zinazohusu matatizo yao katika jamii.

Anasema, wapo waliokuwa na nafasi ya kukemea ufisadi ndani ya serikali lakini wakakaa kimya na kwamba, watu wa namna hii kama walikuwa serikalini walishindwa, ni kipi kinachoweza kuwafanywa wananchi wawaamini?

“Rushwa ndio changamoto kubwa, sarafu inashuka, rasilimali zinaporwa, wananchi wanahangaikia huduma za jamii na huyu anayekuja leo kutoka chama hicho alipaswa kuonesha kuchukia kwa vitendo lakini walaa!.

“Hao hao walipokuwa ndani walishindwa kukemea rushwa inayosababisha umasikini lakini huku nje wanapiga kelele kwamba wanachukia rushwa,” amesema.

Ameongeza “Mtu wa namna hii hata akija na punda ili kudanganya wananchi, hafai na wala hakuna kuangalia sura. Kama mtu hatukumwona akisimamia ajenda za wananchi, huyo hafai kabisa,” anasema Dk. Lwaitama.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine-Mwanza (SAUT), Dk. Francis Ng’atigwa, anasema, kitu kinachoweza kuwaweka wasaka madarasa hao ni kubeba ajaenda za vyama vya na sio zao binafsi.

Anasema kuwa, sera ndio zinazoonesha vipaumbela kwa wagombea hao na si kitu kingine. “Wananchi wanahitaji kusikia sera na sia ajenda binafsi za wagombea. Naamini wagombea wanaobeba ajenda zao binasi watapotea kwa kukosa ‘support’ (kuungwa mkono),” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislam cha Morogoro, Bagesi Gaddafi, anasema jambo la msingi kwa wanansiasa ni kujua matatizo ya wananchi na si kutumia fedha, vitisho na ghiliba isipokuwa ni kuonesha uwezo halisi.

Anasema kuwa, haamini kama Watanzania bado wapo kwenye giza kwa kufuata mkumbo ama mdundo wa sauti unakovuma pasipo sababu.

“Sidhani kama tupo kwenye zama hizo, zama za sasa ni zama za kuchanganua mambo. Kwa bahati nzuri vyama vya upinzania vimekita mizizi kwa kiwango cha kutosha,” anasema Gaddafi.

Mhadhiri huyo anasema kuwa, siasa za Tanzania kwa sasa zina sura tofauti. ”Sura iliyopo ni ya kuhoji na kutaka majibu ya hapo kwa hapo.

“Unaweza kuona tu uchaguzi wa Serikali za Mitaa matokeo yake, angalia watu wa vijijini wanavyokesha kusubiri kuandikwa katika daftari la wapiga kura, hapa ndio unaweza kutathmini tuelekeako,” amesema.

Uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais umepangwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, na tayari makada wa vyamba mablimbali wanaendelea na hekeheka za kutangaza nia pamoja na kuchukua fomu kuomba kuteuliwakuwa wagombea.

error: Content is protected !!