MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amekamatwa na polisi eneo la viwanda (EPZA) Mabibo kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda. Anaandika Josephat Isango … (endelea).
Tukio hilo limetokea kukiwa na mgomo wa wafanyakazi zaidi ya 1800 wa kiwanda cha nguo cha TZ TOOKU ambao walimpigia mbunge wao aende kutatua mgogoro huo.
Kubenea alifika katika eneo hilo saa 6 mchana, akakutana na wafanyakazi kusikiliza kero zao za muda mrefu.
Kisha aliamua kuondoka na viongozi wa wafanyakazi hao na kufanya kikao na menejimenti ya kiwanda hicho kuanzia saa 7 hadi saa 9.
Ilipofika saa 10:30 Makonda alikuja na kupata taarifa kwa muafaka uliofikiwa kati ya Kubenea, menejimenti na viongozi wa wafanyakazi.
Alitoa amri wafanyakazi wakusanyike, akaawaambia kesho atafika huko na Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Kazi na Ajira, na Waziri wa Afya Wanawake, Jinsia na Watoto.
Baada ya kutoa maagizo hayo, Makonda alimzuia Mbunge asihutubie kuaga wananchi aliokuwa nao tangu mchana, kutokana na hali hiyo Kubenea alisema ni vema aseme neno, ndipo mvutano ulipoanza.
Makonda alimuru mkutano ufungwe lakini wafanyakazi hawakutawanyika eneo hilo, alipoona hivyo aliamrisha Polisi wamkamate Kubenea, kwa madai alimwita yeye Kibaka.
Katika tukio hilo, Mwandishi wa habari wa Star Tv aliyekuwa anarekodi tukio hilo alinyang’anywa kamera na Polisi aliyejulikana kwa jina moja tu la Denis.
Mwandishi wa habari hii alijaribu kumsaidia mwenzake ili arejeshewe kamera lakini Polisi wa kituo cha Magomeni walimtisha, na kumtaka kuondoka haraka huku wakiondoka na aliyenyang’anywa kamera.
Baada ya Kubenea kushikiliwa na Polisi kwa zaidi ya saa tano na kuandika maelezo chini ya mwanasheria wake, Fred Kihwelo aliachiwa saa 4 usiku kwa dhamana.
Hiyo ndiyo Tanzania imejaa viongozi wahuni. Sasa amekamatwa kwa kosa gani? Na kwanini polisi wamnyang’anye mwandishi wa habari Camera? Hivi hao viongozi wanaapishwa ili iweje wakati wamejaa uongo na hawana uaminifu?
Mimi pia nimeudhika kwa kitendo hiki cha Makonda na polisi. Mbunge ana wajibu wa kukutana na kuongea na wananchi katika jimbo lake. Ana haki ya kufanya hivyo. Ni udikteta na utovu wa busara kumzuia mbunge katika kutekeleza wajibu wake huo, hasa nikizingatia taarifa kuwa alikuwa ameombwa kwenda kuongea na wafanyakazi. Kitendo cha kunyang’anya kamera ya mwanahabari ni hujuma nyingine. Mwanahabari ana wajibu wa kufanya katika jamii. Wajibu huo uheshimiwe. Na raia wana haki ya kupata habari zinazoihusu jamii. Tangazo la kimataifa la haki za binadamu linatamka wazi kuwa kila binadamu ana haki ya kutafuta, kupata, na kusambaza habari. Polisi wajielimishe kuhusu haki za binadamu na waziheshimu.